MIFUGO
Ufugaji ni shughuli kuu muhimu ya pili ya uchumi baada ya kilimo katika Mkoa. Takribani asilimia 51 ya kaya hujishughulisha na ufugaji. Mifugo inayofugwa kwa wingi ni ng’ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe, kuku na punda.
Mkoa unakadiriwa kuwa na ng’ombe 664,471 mbuzi 185,931 kondoo 56,291 nguruwe 44,177 na kuku 422,937. Wanyama wengine ni pamoja na punda 10,824, bata 33,935, kanga 10,222, mbwa 41,159 na paka 9,514.
Maeneo ya ufugaji yanayotambuliwa kwa kupimwa na kumilikiwa kisheria ni hekta 79,884.63 za Mashamba makubwa ya mifugo ambayo ni Ranchi ya NARCO Kalambo, SAAFI Ltd na Efatha Heritage. Maeneo mengine yanayotumika kwa ufugaji tu vijijini yanakadiriwa kufikia hekta 85,452.2. Mashamba ya kilimo hutumika kama sehemu ya malisho mara baada ya kuvunwa kwa mazao.
Masoko na Biashara ya mifugo hai na mazao ya mifugo
Katika kipindi cha Julai, 2017 hadi June, 2018 biashara ya mifugo imewaingizia wafugaji na wafanya biashara ya mifugo kiasi cha fedha zinazokadiriwa kuwa jumla ya Sh. 26,469,492,500 kutokana na kuuza Ng’ombe 47,385, Mbuzi 14,912, Kondoo 2,255, Nguruwe 6,118 na Kuku 203,553.
Jumla ya ng’ombe 31,659, mbuzi 1,595, kondoo 582, nguruwe 1,672, punda 46, nyatimaji 1, farasi 4 na sungura 40 walisafirishwa ndani ya nchi. Ng’ombe 3,395 na nguruwe 2 walisafirishwa kwenda nje ya nchi (Zambia). Nyama iliyozalishwa katika uchinjaji ilikuwa ni tani 3,456.3 yenye thamani inayokadiriwa kuwa ni Sh. 17,181,815,300 ambapo ng’ombe 15,734, mbuzi 17,327, kondoo 2,816 na nguruwe 9,668 walichinjwa. Maziwa kiasi cha lita 3,845,095 yenye thamani ya Sh. 2,406,984,350 yaliuzwa. Jumla ya mayai trei 83,546 yenye thamani ya Sh. 891,266,700 yaliuzwa. Kadhalika, jumla ya vipande 13,256 vya ngozi ghafi vyenye thamani ya Sh. 10,041,800 viliuzwa.
Usajili na utoaji Leseni kwa wafanyabiashara wa mifugo na nyama
Kwa mujibu wa Sheria ya Tasnia ya Nyama wafanyabiashara wote wanaofanya biashara ya kununua na kuuza mifugo katika minada ya mifugo, wanaosafirisha mifugo na wanaouza nyama ndani na nje ya nchi wanapaswa kujisajili Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) na kupata leseni rasmi kulingana na aina na ngazi ya biashara na usafirishaji wa mifugo na nyama ndani au nje ya nchi. Wakati wa doria zilizofanywa na Kikosi cha Wizara ya Mifugo na Uvuvi kati ya tarehe 26 Machi na 31 Aprili, 2018 ilibainika kuwa wafanyabiashara hawajasajiliwa na TMB na wengi hawana leseni halali. Kufuatia hali hiyo tarehe 3.5.2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ilichukua jukumu la kutoa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu Sheria, Kanuni na Taratibu zinazohusiana na tasnia ya nyama. Hadi kufikia Agosti 17, 2018, wafanyabiashara waliojisajili TMB kwa ajili ya bucha ni 12 na kwa ajili ya kununua na kusafirisha mifugo ni 21. Wafanyabiashara waliopata leseni za kununua na kusafirisha mifugo ngazi ya mkoa ni 9, ngazi ya kitaifa ni 1 kati ya wafanyabiashara 21 waliotuma maombi ya leseni. Ufuatiliaji unaendelea.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa