TAARIFA ZA ELIMU
Utangulizi
Mkoa unafanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha kuwa kiwango cha elimu, kuanzia elimu ya Awali, Msingi, Sekondari, ufundi na Elimu ya Watu Wazima, kinaboreshwa kwa kuhakikisha kuwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa. Vile vile kusimamia suala la mahudhurio na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Mwaka 2023, Mkoa wa Rukwa unazo Jumla ya Shule 506, kati ya hizo Shule za Awali na Msingi 399 na Shule za Sekondari 107. Kati ya Shule za msingi, Shule 382 ni za Serikali na Shule 17 sio za Serikali na kati ya Shule 107 za Sekondari, Shule 81 ni za Serikali na Shule 26 sio za Serikali. Mkoa pia unazo taasisi za Elimu ya kati na juu kama ifuatavyo: Vyuo 12 Elimu ya Kati kati ya Vyuo hivyo, Vyuo Vitani ni vya Serkali na Vyuo Saba sio vya Serikali. Mkoa unavyo Vyuo Vikuuu 2 vya Serikali ambavyo ni Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) tawi la Rukwa na Mbeya University of Science and Tecnology MUST- Rukwa Branch. Aidha, Chuo kimoja cha VETA kinaendelea kujengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo.
Mkoa unalo jukumu la kuratibu na kusimamia uendeshaji wa Shule za Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari, vyuo vya Ufundi stadi na Elimu ya Watu Wazima. Aidha, jukumu lingine ni kuhakikisha kuwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa na kumaliza mzunguko wa Elimu, ngazi husika pia kusimamia uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Elimu ya Awali na Msingi
Katika mwaka 2023, uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya awali na msingi unaonesha kuwa, idadi ya Wanafunzi katika Shule za Msingi darasa la Awali hadi VII ni 349,801 (Wavulana:167,836, Wasichana :181,965) na mahitaji ya Walimu ni 7,707 wakati waliopo ni 4,283 na kuwa na upungufu wa walimu 3,424 sawa na 43.75%.
Elimu ya Sekondari
Katika mwaka wa 2023 idadi ya Wanafunzi kwa Shule za Sekondari za Serikali ni 58,666 wakiwemo wavulana 28,953 na wasichana 29,713. Idadi ya Walimu wanaohitajika ni 2,382, kati ya hao Walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati ni 959 na masomo ya Sanaa, biashara na Lugha ni 1,423. Walimu waliopo ni 1,548 ambapo Walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati ni 506 na wa Masomo ya Sanaa, Biashara na Lugha ni 1,042. Mkoa una upungufu wa Walimu 834 kati yao walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati 453 sawa na 47.2% na Walimu wa Masomo ya Sanaa, Biashara na Lugha 381 sawa na 26.7%.
Elimu ya Watu Wazima
Katika uboreshaji wa Elimu ya Watu Wazima Mkoa una vituo vya Walimu (Teachers Resource Centres) 6, vituo hivi hutumika kuongeza na kubadilishana uzoefu na maarifa kwa Walimu ili kuboresha ufundishaji na utoaji wa maarifa kwa Wanafunzi. Mkoa unatekeleza program ya Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (MEMKWA) Mkoa una vituo 55 vya MEMKWA katika Halmashauri 4 za Mkoa wa Rukwa. Hapo awali vituo vilikuwa vinafadhiliwa na program ya LANES, lakini kwa sasa vipo chini ya Halmashauri tangu Mwaka 2018 Vituo vyote vina jumla ya wanafunzi 2,065 wakiwemo wavulana 1,033 na wasichana 1,032
Mpango wa kuboresha Elimu ya Sekondari ni program ya Elimu Nje ya Mfumo Rasmi ambayo inatoa mafunzo kwa wasichana walikatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito. Mkoa una vituo Vitatu (3) vyenye jumla ya wanafunzi 232 vinavyotoa Elimu ya Sekondari kupitia program ya SEQUIP-AEP. Kituo cha Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kilichopo Manispaa ya Sumbawanga chenye jumla ya wanafunzi 142. Kituo cha Pili kipo Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kiitwacho Matai Open School chenye jumla wa wanafunzi 67 na kituo cha tatu ni Mpui chenye wanafunzi 23.
Mkoa wa Rukwa ulianza unatekeleza Mpango Endelevu Changamani kwa Vijana (MECHAVI) yaani Integrated Program for Out of School Adolescent – (IPOSA). Mpango huu unafadhiliwa na asasi isiyo ya Serikali ya Rafiki Social Development Organization (RAFIKI - SDO) Mpango unatekelezwa katika Halmashauri tatu za Kalambo, Nkasi na Sumbawanga, Mkoa una jumla ya vituo 15 na vijana walioandikishwa ni 167 Wanaume 52 na wanawake 115
Mkoa una vikundi vitano vya MUKEJA vilivyosajiliwa vilivyo chini ya kitengo cha Elimu ya Watu Wazima vyenye jumla ya wanakisomo 75. Vikundi hivi vipo katika Halmashauri za Wilaya ya Kalambo na Nkasi
Elimu Maalum
Mkoa una shule 1 ya Elimu Maalum ambayo ni Shule ya Msingi Malangali iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga. Shule hii ina jumla ya wanafunzi 92 wenye aina mbalimbali za ulemavu. Aidha, Mkoa una Vitengo 24 vinavyotoa Elimu maalum na shule 376 Jumuishi. Vilevile kuna Shule 1 ya Sekondari ya Kantalamba inayotoa Elimu Maalum iliyopo katika Manispaa ya Sumbawanga. Mkoa una jumla ya wanafunzi 1,701 wenye mahitaji maalum kulingana na aina mbalimbali za ulemavu.
Elimu ya Ualimu na Vituo vya Ufundi Stadi
Mkoa una jumla ya Vyuo vya Ualimu viwili (2) ambapo Chuo cha Ualimu Sumbawanga kinamilikiwa na serikali na Chuo cha Ualimu St. Maurus kinamilikiwa na taasisi isiyo ya kisekali. Aidha, Mkoa una Vituo vitatu (3) vya Ufundi Stadi vinavyomilikiwa na serikali vilivyopo katika shule za msingi za Mwazye, Matai na Katandala “B.”
Vyuo vya Ufundi
Katika uboreshaji wa Elimu ya Ufundi Mkoa una vyuo vitano vinavyotoa Elimu ya Ufundi Stadi ambavyo ni Furaha Center, Katandala VTC, Chala FDC, Paramawe VTC na Mvimwa VTC, St. Anselmo VTC Chala. Aidha, Mkoa unaendelea na jitihada za kuhakikisha Chuo Kikubwa na cha kisasa cha VETA kinakamilika kujengwa katika Manispaa ya Sumbawanga eneo la Kashai (Muva) ambapo ujenzi umefikia 98% Baada ya ujenzi kukamilika chuo hiki kitakuwa na uwezo wa kuchukuwa wanafunzi 1500 kwa mkupuo (600 wa bweni na 900 wa kutwa) wa kozi za muda mrefu na muda mfupi. Mafunzo yanayotolewa ni ya ufundi magari, umeme, uselemala, uashi, uchomeleaji wa vyuma, uhazili, ubunifu wa mavazi, ukarimu na usindikaji wa vyakula.
Elimu ya Chuo Kikuu
Mkoa una kituo cha Chuo Kikuu Huria kilichopo Manispaa ya Sumbawanga. Pia, Chuo Kikuu cha Sayansi Tawi la Sumbawanga (Mbeya University of Science and Technology- MUST) kilichopo katika eneo la Mtapenda katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. Chuo hiki kina Chti cha Ithibati ya Usajili Na. CR1/026; kilianza udahili mwaka wa masomo 2019/2020.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa