SEKTA YA UVUVI
Hali ya uvuvi Mkoani
Mkoa una idadi ya wananchi 14,094 wanaojishughulisha moja kwa moja na uvuvi na wananchi 1,021 wanaojishughulisha na uchakataji wa mazao ya uvuvi. Wavuvi wanamiliki mitumbwi ya uvuvi 2,820. Katika Mkoa, shughuli za uvuvi zinafanyika kwa kiasi kikubwa katika maziwa mawili makubwa ambayo ni Ziwa Tanganyika na Rukwa na kwa kiasi kidogo katika maziwa madogo mawili ya asili ambayo ni Kwela na Sundu. Halikadhalika Uvuvi hufanyika katika mito 87 na mabwawa 326 yaliyochimbwa na wananchi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa.
Katika kipindi cha mwaka 2018/2019 jumla ya tani 2,976.75 zenye thamani ya shilingi bilioni 12.9 zilivunwa na kusafirishwa ndani na nje ya Mkoa. Fedha hizi ni mapato yaliyotokana na uvuvi wa samaki katika maeneo mbalimbali ya Mkoa.
Ujenzi wa soko la samaki la Kasanga
Ujenzi wa soko la samaki la Kasanga umegharamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kwa kushirikiana na Muungano wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA), Jumuia ya Ulaya (EU), Shirika la Usimamizi wa miradi ya Jumuia ya Ulaya (GRET), Jamii ya Kasanga, MIVARF na Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Wadau wote hawa wamekwishachangia jumla ya Shilingi 1,408,856,527/= katika ujenzi wa miundo mbinu ya soko hili. Katika kipindi cha mwaka 2018/2019 Mkoa kwa kushirikiana na MIVARF umeweka vyumba baridi( cold rooms) na mtambo wa kuzalisha barafu (ice plant).Vifaa hivi vitawawezesha wavuvi wetu kuhifadhi mazao yao ya uvuvi kwa muda mrefu bila kuharibika huku wakisubiri soko la uhakika.
Mwalo wa samaki wa Kirando
Ujenzi wa Mwalo wa Kirando umefadhiliwa kwa pamoja na Programu endelevu ya bonde la Ziwa Tanganyika (PRODAP) na MIVARF ambapo PRODAP imechangia jumla ya Shilingi 648,385,505/= na MIVARF imechangia shilingi 357,807,500/=. Mwalo unaendelea kutoa huduma kwa Wavuvi na Wafanyabiashara wa Samaki na dagaa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa