Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameiagiza Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Rukwa kumchukulia hatua za kinidhamu Afisa uhamiaji wa Wilaya ya Nkasi aliyechukua Rushwa ya Shilingi 315,000/= kutoka kwa wahamiaji wa nchi ya Burundi aliyekuwa anapita nchini kuelekea nchi za kusini mwa Afrika.
Mh. Wangabo amesema kuwa serikali haiwezi kukubali mtumishi mmoja kuvichafua vyombo vya ulinzi na usalama na kuongeza kuwa mtumishi huyo anatakiwa kuwa fundisho kwa maafisa wengine wa vyombo hivyo kwani wao ndio wanatakiwa kuwa mfano wa kuigwa aktika kutii sheria na sio kinyume chake.
“Ni lazima achukuliwe hatua kali sana huyu mtumishi na sielewi ni kwanini hajachukuliwa hatua hizo za nidhamu mpaka sasa hivi, na iwe fundisho kwa mafias wengine kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, ni lazima waonyeshe mfano kwa watu engine lakini sio unakuwa mfano wa kuchukua fedha chafu,” Alisisitiza.
Kwa upande wake Mkuu wa Tasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Rukwa Hamza Mwenda amesema kuwa fedha hizo zimerejeshwa na Afisa Uhamiaji wa Wilaya ya Nkasi baada ya TAKUKURU kubaini kuwa mtumishi huyo alipokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa wahamiaji wa nchi ya jirani.
“Wahamiaji hao walikuwa wakisafiri kwa kwa basi kupitia nchini mwetu kwenda nchi za kusini mwa Afrika wakiwa na vibali vyote na kueleza kuwa alipokea fedha hizo kama zawadi, pamoja na kuchukuliwa hatua za kinidhamu, alitakiwa kurejesha fedha hiyo ambayo itaingizwa kwenye akaunti maalum ya Benki kuu,” Alisema.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa