SENDIGA: SIJARIDHISHWA NA USIMAMIZI MIRADI YA AFYA KALAMBO
Na. OMM Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga amemwelekeza Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Tano Mwera na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Shafii Mpenda kujitafakari juu ya namna wanavyosimamia miradi ya ujenzi wa vituo vya afya kutokana na kutokamilika kwa wakati .
Ameagiza hayo leo (Alhamisi Oktoba 20,2022) kwa nyakati tofauti alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya sekta ya afya wilaya Kalambo pamoja na kuongea na wananchi kusikiliza kero na shida zao.
Sendiga ametembelea na kukagua vituo vinne ambavyo ni kituo cha afya vya Kanyezi (Milioni 400), Legeza Mwendo (Milioni 700), Mwazye (Milioni 500) na hospitali ya wilaya ya Kalambo (Bilioni 3) ambavyo kwa pamoja vimeshatumia zaidi ya shilingi Bilioni 4.6 lakini huduma bado hazijaanza kutolewa .
“Sijafurahishwa kabisa kuona vituo vya afya vilivyokaa miaka zaidi ya minne kutokamilika wakati serikali imetoa fedha. Tatizo hapa nimebaini ni viongozi na watendaji wangu kutosimamia miradi hii ya wananchi" alisema Sendiga.
Sendiga aliongeza kusema “ Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi lazima mkae chini na kujitafakari wilaya hii ina nini? , Kalambo kuna shida kubwa miradi haikamiliki kwa wakati. Siwezi kukubali kuona miradi yenu ikikwama” alisema Mkuu huyo wa Mkoa wa Rukwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Sunday Wambura ilionesha kuwa vituo hivyo vilianza kujengwa mwaka 2018.
Naye Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Legeza Mwendo Dkt. Emanuel Matinda alisema changamoto kwenye miradi ya ya afya ni upatikanaji wa fedha za ndani ya halmashauri kukamilisha kazi ndogo kama za mifumo ya maji taka, umeme na jengo la upasuaji ili huduma kwa wananchi zianze kutolewa.
Naye mkazi wa Matai Mwasulu Abel akizungumza kwenye mkutano wa hadhara alisema vituo vingi vya afya havifanyi kazi icha ya serikali kutoa fedha nyingi hatua inayoleta kero kwa akina mama na watoto.
Mkuu wa mkoa huyo wa Rukwa ametoa agizo kuwa viongozi hao wa wilaya wahakikishe katika kipindi cha siku kumi na nne (14) huduma za afya zianze kutolewa kwenye vituo hivyo vya afya wilayani Kalambo.
Mwisho.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa