RC SENDIGA: WANANCHI ASILIMIA 65 WAPATA CHANJO YA UVIKO-19
Na. OMM Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga amesema katika kukabiliana na janga la Ugonjwa wa UVIKO-19 mkoa umefanikiwa kuongeza uchanjaji kutoka asilimia 23 mwezi Agosti hadi asilimia 65 mwezi huu Oktoba 2022.
Sendiga amesema hayo leo mjini Sumbawanga wakati Akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) ambapo amewapongeza wataalam wa afya kwa jitihada hizo za kuhakikisha wananchi wengi wanapata chanjo ya UVIKO-19.
“Kazi iliyofanyika si ndogo. Pongezi kwa Mganga Mkuu wa Mkoa, Wakurugenzi na timu za Afya kuanzia ngazi ya kaya kwa kufanikisha uchanjaji wa chanjo dhidi ya UVIKO-19” alisema Sendiga.
Sendiga aliongeza kuwa ili jamii iwe salama zaidi hakuna budi uchanjaji ufikie asilimia 75 ambapo wananchi wengi watakuwa na kinga dhidi ya ugonjwa wa korona.
Katika hatua nyingine Sendiga aliwatoa hofu wananchi kuwa mkoa wa Rukwa licha ya kuwa pembezoni bado upo salama na kuwa hakuna tishio la ugonjwa wa Ebola na kuwa tahadhari na elimu kwa umma inaendelea kutolewa.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa Rashid Mchatta alisema watumishi katika sekta mbalimbali wataendelea kutoa huduma kwa wananchi ili kutimiza malengo ya Serikali kuwaletea maendeleo wananchi.
Mwisho.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa