Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo amewataka wajasiliamali wote mkoani humo kujitokeza kupatiwa vitambulisho vya ijasiliamali vilivyotolewa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa mikoa na wilaya zote nchini ili kuwaepusha wajasiliamali hao na bughudha wanazozipata katika kuendesha biashara zao za kila siku.
Amesema kuwa kila halmashauri kati ya halmashauri nne za mkoa wa Rukwa ilipatiwa vitambulisho 6,250 katikati ya mwezi Disemba mwaka 2018 lakini hadi kufikia leo katikati ya mwezi wa kwanza vitambulisho vilivyogawiwa havizidi 150 kwa mkoa mzima hali iliyopelekea Mh. Wangabo kuahirisha ziara ya siku nne aliyopanga kuifanya katika halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ili kujionea miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Nawataka waende katika halmashauri zote haraka iwezekanavyo vinginevyo watakosa hii nafasi ya kuapata vitambulisho na kitakachofuata kinaweza kisiwe kizuri kwa wajasiliamali, kwasababu hiki ni kitambulisho ndicho kinachomfanya mjasiliamali huyu mdogo atambulike na asibughudhiwe kama mheshimiwa rais alivyosema, sasa usipopata kitambulisho maana yake ni kinyume chake ndicho kitakachokuja, unapata kitambulisho ili usibughudhiwe, lakini wewe hujapata kitambulisho inamaana utabughudhiwa, mimi nisingependa wajasiliamali wapate bughudha,” Alibainisha.
Ameyasema hayo baada ya kupata taarifa ya Wilaya ya Kalambo juu ya miradi mbalimbali ya kimaendeleo, mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza, ukusanyaji wa mapato na matumizi ya halmashauri, ugawaji wa vitambulisho hivyo pamoja na hali ya kilimo ya Wilaya kabla ya kutaka kuanza ziara yake katika wilaya hiyo.
Aidha amesisitiza kuwa tathmini ya ugawaji wa vitambulisho hivyo itafanyika baada ya siku kumi tangu leo tarehe 15.1.2019 hadi tarehe 25.1.2019 ili kuona muitikio wa wajasiliamali hao kwa halmashauri zote na kuwaagiza wakurugenzi wa halmashauri hizo kuhakikisha wanaongeza kasi ya kuwasajili na kuwakabidhi wajasiliamali hao vitambulisho vyao bila ya bughudha yoyote.
Wakati akiwasilisha taarifa ya wilaya, katibu tawala wa wilaya ya Kalambo Frank Sichalwe alisema kuwa tangu kufanyika kwa uzinduzi wa ugawaji wa vitambulisho hivyo mwanzoni mwa mwaka huu ni wajasiliamali kumi tu ndio waliopatiwa vitambulisho hivyo pamoja na kuendelea na hamasa ya kuwatambua wajasiliamali wengine.
“Zoezi la hamasa na ugawaji wa vitambulisho linaendelea ili vitambulisho vingi zaidi viweze kutolewa na kuwanufaisha wajasiliamali katika sekta isiyorasmi kama mheshimiwa Rais alivyokusudia, mpaka sasa Ulumi tumepata wajasiliamali 80, Mwimbi 30, Kasanga 30, Mwazye 20 na Matai wamejitokeza wajasiliamali zaidi ya 100 mpaka sasa,” Alisema.
Vitambulisho vya ujasiliamali viligagiwa kwa wakuu wote wa mikoa 26 mwanzoni mwa mwezi Disema mwaka 2018 na kila mkoa kupata vitambulisho 25,000 ili kuweza kuvigawa kwa wakuu wa wilaya na hatimae kufika mikononi mwa wakurugenzi ili kuwapatia wahusika wa vitambulisho hivyo kwa lengo la kupunguza bughudha kwa wajasiliamali wataopata vitambulisho hivyo vyenye gharama ya shilingi 20,000 kwa kila kitambulisho.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa