Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameiagiza kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga kuhakikisha wanashirikiana na Halmashauri kupunguza idadi ya mifugo iliyopo kwenye halmashauri hiyo ili kudhibiti utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na hifadhi za misitu na kuliokoa ziwa Rukwa.
Amesema kuwa shughuli hizo za ufugaji karibu na vyanzo vya maji ndizo zinazopelekea kujaa kwa tope katika ziwa Rukwa, ziwa linaloasisi jina la Mkoa huo na kuongeza kuwa serikali haipo tayari kuona ziwa hilo likipotea na kusisitiza kuhifadhiwa kwa namna yoyote ile ikiwemo kupiga marufuku kufanbya shughuli za ufugaji kwenye vyanzo vya maji.
“Nashkuru kwamba zoezi la kupiga chapa linaendelea ila baada ya kumaliza zoezi hilo muanze kwenda boma kwa boma muhakikishe kwamba animal Unit “idadi ya mfugo kwa eneo” inazingatiwa, mtu ashauriwe kupunguza mifugo yake au ahame akatafute mahali pengine, kwasababu hatuwezi kujaza mifugo kwenye bonde la ziwa Rukwa halafu ziwa likafutika, serikali haitakubali.” Alibainisha.
Ameyasema hayo baada ya kusomewa taarifa ya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga katika Ziara yake ya siku mbili yenye lengo la kutembelea miradi mbalimbali, kujitambulisha kwa watumishi pamoja na kuongea na makundi mbalimbali ya wananchi katika halmashauri hiyo.
Katika taarifa hiyo ilionesha kuwa idadi ya wanyama iliyopo katika bonde hilo ni 143,346 huku idadi inayotakiwa ni 36,666 huku ikionesha kuongezeka mara tatu zaidi ya mahitaji ya uwepo wa Wanyama hao katika bonde hilo.
Katika kulisisitiza hilo Mh. Wangabo amewatahadharisha wananchi kufuga kisasa kwa kuwa na mifugo michache yenye kuleta tija huku ikizingati uhitaji wa ardhi kwaajili ya kilimo na shughuli nyingine za kibinaadamu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa skimu ya umwagiliaji Kijiji cha Ng’ongo, kata ya Mtowisa Wilayani Sumbawanga, Justin Amon amesema kuwa wafugaji wamekuwa wengi katika bonde hilo hasa katika skimu yao hiyo na kuwasababishia hasara pale wanapopeleka mifugo yao kwaajili ya malisho.
“Kama taarifa ilivyosomwa wafugaji wapo wengi ambao wamegeuza eneo hili kuwa sehemu ya machungio, tunapojaribu kuwafuatilia wanatushishia na mawe, fimbo, sime na mapanga na wapo tayari kupambana kwa lolote litakalotokea, na kesi zipo mahakamani lakini tunaambiwa hatujakamilisha vigezo, hivyo tunashindwa na kushindwa kujua kwamba tunasaidiwaje na serikali yetu, wafugaji wanatunyanyasa sana,” Alisema.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa