Serikali Mkoani Rukwa imewataka wawekezaji katika viwanda vya uzalishaji wa chakula kuongeza uzalishaji wa chakula chenye virutubisho muhimu ili kupunguza changamoto ya udumavu inayotokana na lishe duni.
Hayo yamesemwa wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa kipindi cha Julai 2023- Juni 2024 kilichofanyika tarehe 29 Agosti 2024 katika ukumbi wa RDC ulioko katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Kikao hicho kilichoongozwa na Mheshimiwa Peter Ambrose Lijualikali kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere kimeshauri kila Halmashauri kuweka mkakati maalum wa kuongeza idadi ya viwanda hatua itakayoongeza kiwango cha uzalishaji wa chakula chenye virutubisho.
Mheshimiwa Lijualikali ameeleza kuwa, kuanzishwa na kuimarishwa kwa viwanda vinavyochakata chakula vyenye virutubisho ni hatua muhimu katika kuboresha afya na ustawi wa wananchi, hasa watoto na wanawake wajawazito ambao wako katika hatari kubwa ya kukumbwa na matatizo udumavu.
Wajumbe wa Kikao hicho wameshauri kuwa mkakati huo ushirikishe sekta ya kilimo, viwanda, afya, na wadau wa maendeleo, kwa lengo la kujenga uwezo wa ndani wa uzalishaji na usambazaji wa chakula vyenye virutubisho.
Mheshimiwa Lijualikali ameeleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji na wadau mbalimbali ili kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa na unaleta matokeo yanayotarajiwa ikiwa ni sehemu ya juhudi ya Mkoa wa Rukwa kuhakikisha kuwa mkataba wa lishe unatekelezwa kikamilifu.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa