Balozi wa Kenya nchini Tanzania Dan Kazungu amewaomba wawekezaji kutoka kila pande ya dunia kujitokeza kwa wingi kuwekeza kwa kujenga hoteli na nyumba za kupumzikia wageni katika eneo linalozunguka maporomoko ya Kalambo (Kalambo Falls) yaliyopo katika Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa.
Amesema kuwa eneo hilo ni zuri kwa wanafamilia kulitumia katika siku za mapumziko, siku za sikukuu na pia kujitokeza ili kuyaona maajabu hayo ambayo yametambuliwa na Shirika la umoja wa mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni (UNESCO) kuwa ni urithi wa dunia.
“Tunaomba wawekezaji waje hapa kwa wingi, hapa kuna kivutio ambacho kimejulikana na umoja wa mataifa UNESCO kama hifadhi ya urithi wa dunia, mje wawekezaji hapa, pahali ambapo siku za mwisho wa wiki watu wanaweza kuja kujipumzisha ama siku za sikukuu kuja na familia yao kwaajili ya “picnic”, wanajenga “lodges” lakini tunaomba “lodges” zijengwe nyingi zaidi za hadhi ya ubora wa juu zaidi ili tufurahie na familia zetu,” Alisema.
Balozi Kazungu ameyasema hayo alipotembelea maporomoko ya kalambo katika ziara yake ya siku moja Mkoani Rukwa iliyolenga kutafuta fursa za uwekezaji katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huku akitembelea kiwanda cha Nyama cha SAAFI pamoja na ujenzi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Sumbawanga.
Aidha, Balozi Kazungu alitoa ushauri kwa wakala wa misitu Tanzania wanaoshughulika na uhifadhi wa msitu wa Kalambo pamoja na kuimarisha miundombinu ya maporomopko hayo kuona uwezekazo wa kuweka nyaya pamoja na vigari vitakavyopita kwenye nyaya hizo ili watalii waweze kuyaona maporomoko hayo vizuri zaidi pamoja na msitu huo.
Wakati akisoma taarifa ya maporomoko hayo ya Kalambo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Misitu Wilaya ya Kalambo Helman Ndanzi amesema kuwa pindi ujenzi wa ngazi za kushukukia kutoka maporomoko yanapoanzia hadi kufikia sehemu maji yanapodondokea utakapokamilika, ngazi hizo zitakuwa na urefu wa mita 1277 na kugharimu shilingi 852,789,066.70.
“Changamoto zilizopo ni kutotangazwa vya kutosha maporomoko hayo hali inayopelekea kutojitokeza kwa wawekezaji katika eneo hilo ambalo mawasiliano ya simu pia bado ni tatizo na hivyo tunaiomba mitandano mbalimbali ya simu kujitokeza kuweka minara katika maeneo haya ili mawasiliano yawe rahisi,” Alisema.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alimhakikishia Balozi huyo kuwa mkoa umejipanga kuhakikisha unakamilisha miundombinu inayohitajika ili kuwarahisishia wawekezaji kutekeleza shughuli zao kwa urahisi na hatimae kuinua uchumi wa wananchi katika mkoa lakini pia uchumi Tanzania kwa ujumla.
“Sisi tupo kwenye mpango ule wa viwanja vya ndege vile vinne, kuna kiwanja hiki cha Sumbawanga, Tabora, Shinyanga pamoja na Kigoma, karibu kila kitu kipo tayari kimazingira, vitu vyote vinavyotakiwa kufanyika kabla ya kuanza upanuzi wa uwanja tayari vimekwishafanyika, mhandisi mshauri yupo, mkandarasi yupo, mikataba tayari, fidia kwa wananchi waliohusika nae neo la upanuzi tayari, kila kitu kipo tayari, bado serikali haijaruhu lakini bila ya shaka wakati wowote ruhusa itatoka,” Alisisitiza.
Maporomoko ya Kalambo ni maporomoko ya pili kwa urefu kutoka maji yanapoanzia kumwagika hadi yanapodondokea kwa mita 235 na upana wa mita kuanzia 3.6 hadi mita 18 (single drop waterfall) ambapo maporomoko ya kwanza ni ya TUGELA yaliyopo Afrika ya Kusini yenye urefu wa mita 947.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa