Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mheshimiwa Charlotta Ozaki Marcias, amefanya ziara ya siku tatu ya ukaguzi wa miradi inayofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la SNV la Sweden kupitia Mradi wa Sustain Mkoani Rukwa.
Katika ziara hiyo, iliyofanyika kuanzia tarehe 2 hadi 4 Desemba 2024, Mheshimiwa Charlotta Ozaki Marcias amekagua miradi ya kilimo na chakula, usawa wa kijinsia, ushirikishwaji wa jamii, utawala bora, mabadiliko ya tabia nchi na miradi ya maji inayofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la SNV. Pamoja na ukaguzi wa miradi hiyo Mheshimiwa Balozi huyo ameshiriki zoezi la upandaji miti katika eneo la Bwawa la Kwela lililoko Kijiji cha Mshani, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.
Kwa upande wao wananchi wa Mkoa wa Rukwa wameeleza manufaa waliyopata kutokana na mafunzo na ushauri wa kitaalamu kutoka kwa Shirika la SNV. Kupitia mradi wake wa Sustain, Shirika hilo limetoa mafunzo ya ufugaji bora wa nyuki, kilimo na lishe na urejeshaji wa uoto ili kukabiliana na changamoto za utapiamlo, pamoja na urejeshaji na utunzaji wa misitu ili kukabiliana na changamoto za utapiamlo na mabadiliko ya tabia nchi.
Pamoja na manufaa yaliyoelezwa wananchi wamemwomba Mheshimiwa Balozi kuwasaidia katika mchakato wa biashara ya hewa ukaa (carbon credit).
Shirika la Maendeleo la SNV linatekeleza miradi katika vijiji vya Kilembo, Mleche, Kalambanzite, na Mshani vilivyoko Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga huku pia ikitekeleza miradi katika vijiji vya Kachele, Kafukoka, Chisesa, Samazi vilivyoko Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo na vijiji vya Chala B, Chimwa, Isasa, na Nkomolo vilivyoko Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa