Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewasisitiza msimamizi mshauri wa ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kalambo ambao ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kushirikiana na Mkandarasi SUMA JKT kuhakikisha wanamaliza jengo hilo kwa wakati.
Amesema kuwa Ujenzi huo ulisimama zaidi ya miezi minne ambao ulitakiwa kumalizika mwezi wa 5 na kwa uchelewaji huo utasababisha kumalizika mwezi wa 10 jambo ambalo sio matarajio ya serikali ya awamu ya tano kufanya kazi kwa kusuasua.
“TBA wahakikishe wanashirikiana vizuri na SUMA JKT ili kumaliza ujenzi huu na ili hili jengo liende kwa kasi tunayoitaka kila mwezi tutakuwa tunapita kuangalia maendeleo ya ujenzi huo, sijaamini kwamba TBA wameshindwa kuwasimamia SUMA JKT ninachotaka makubaliano yote ya pande mbili yaheshimiwe ili kazi ziende kusiwe na mjuzi zaidi ya mwenziwe, mwelekezane” Mh. Wangabo alibainisha.
Hayo yamejitokeza baada ya Mh. Wangabo kutembelea ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kalambo na kuona kusuasua kwa ujenzi huo na kuamua kuitisha kikao ili kujua sababu za kujitokeza kwa hali hiyo ambayo sio makubaliano na hakuna taarifa za kuridhisha juu ya maendeleo ya ujenzi huo.
Awali akitoa taarifa ya kusuasua kwa ujenzi huo Meneja wa Wakala wa Majengo Mkoa wa Rukwa Arch Deocles Alphonce amesema kuwa ujenzi huo ulitakiwa kumalizika tarehe 16/5/2018 lakini kutokana na sababu za hali ya hewa na mabadiliko ya ramani kutokana na jiografia ya eneo ndio iliyopelekea kuchelewa kwa ujenzi huo kumalizika kwa wakati.
Nao Suma JKT wakimshukuru Mh. Wangabo kwa kuwakutanisha makundi matatu, wao kama Mkandarasi, Mteja ambae ni ofisi ya Katibu Tawala mkoa pamoja na Msimamizi Mshauri (TBA) kuelekezana palipokwenda tofauti na hatimae kufikia muafaka na kuendelea na ujenzi huo wenye thaamni ya Shilingi Milioni 289.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa