BILIONI 27 ZATOLEWA KUBORESHA BARABARA ZA RUKWA- RC MKIRIKITI
Na. OMM Rukwa.
Zaidi ya shilingi Bilioni 27.5 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara zilizo chini ya Wakala za TANROADS na TARURA katika mwaka wa fedha 2021/2022 ikiwa ni ongezeko la kibajeti mara mbili zaidi ya lile la awali kwa mwaka fedha uliopita.
Kutolewa kwa fedha hizo kunatajwa kuwa ni moja ya mafanikio makubwa ya serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan tangia aingie madaraka takribani mwaka mmoja hadi sasa.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha 40 Bodi ya Barabara mkoa hii leo (28.02.2022) mjini Sumbawanga, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti amesema fedha hizo tayari zinaendelea kutekeleza miradi ya barabara kwenye maeneo mbalimbali mkoani humo.
“Nichukue fursa hii kuipongeza serikali yetu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutupatia fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara zetu ambapo maendeleo makubwa yanaonekana kote “alisema Mkirikiti.
Mkuu huo wa Mkoa aliongeza kusema kqti ya fedha hizo shilingi Bilioni 15.2 ni kwa ajili ya barabara za Tanroads na Bilioni 12.3 ni kwa ajili ya barabara za Tarura.
Mkirikiti aliwataka wajumbe wa kikao hicho kufanya tathmini ya kina juu ya matumizi ya fedha hizo za barabara kwa kuwa zimetolewa na serikali kwa lengo la kuboresha barabara hususan za vijijini ili zichochee ukuaji wa uchumi .
“Fedha hizi ni zaidi ya mara tatu ya makusanyo ya halmashauri zetu zote nne. Makusanyo ya ndani ya halmashauri zetu ni Bilioni takribani 9 katika mwaka 2021/22” alisema Mkirikiti.
Aidha, Mbunge wa Kalambo Josephat Kandege aliomba serikali kufanya udhibiti na kulinda eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja mpya wa ndege Kisumba ili wananchi wasilivamie na kwa kilimo na makazi.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji kazi za barabara kuu za mkoa kwa mwaka 2021/22 na mpango na bajeti kwa mwaka 2022/2023 Meneja wa Tanroad Mkoa wa Rukwa Mhandisi Mgeni Mwanga alisema asilimia kubwa barabara za mkoa za lami na changarawe zote zilikuwa na hali nzuri.
Mhandisi Mwanga alisema Tanroad inasimamia mtandao wa barabara zenye urefu wa kilometa 1,250.2 ambapo barabara kuu zina urefu wa kilometa 415 kati ya hizo za lami ni (298.35 km) na changarawe (117.51 km) na barabara za mkoa zina jumla ya kilometa 834.98 kati hizo za lami ni (76.8 km) na za changarawe ni (758.1 km) .
Mhandisi Mwanga alisema katika mwaka 2022/2023 bajeti ya matengenezo kupitia Mfuko wa Barabara inayotarajia kupitishwa na Bunge ni shilingi Bilioni 13.81 ambapo jumla ya madaraja 32 katika barabara kuu na madaraja 62 katika barabara za mkoa yatajengwa na kukarabatiwa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa