BILIONI 55.9 ZALIFUNGUA ANGA LA SUMBAWANGA
Mkataba wa ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Sumbawanga umetiwa saini kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Kampuni ya Beijing Construction Enginering Limited ya China.
Hafla ya kusaini Mkataba huo imefanyika leo tarehe 29 Aprili 2023 huku ukishuhudiwa na Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa ambaye alikuwa mgeni rasmi, wengine ni Mhe. Queen Cuthbert Sendiga ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi Mhe. Sultan Saleh Seif, Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini Mhe. Aeish Hillal Khalfan, Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Bw. Gerald Kusaya, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Rukwa .
Akizungumza na mamia ya wananchi waliokusanyika katika eneo la uwanja wa ndege unaotarajiwa kukarabatiwa Mhe. Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi amemshukuru na kumpongeza Mhe. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutafuta fedha kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya kwa ajili ya ukarabati wa kiwanja hicho cha ndege.
Amesema miundombinu ya uwanja itaruhusu ndege kutua na kupaa usiku na mchana na kwamba uwanja utahudumia na kuunganisha ukanda wa magharibi na mikoa mingine. Mkataba wa ujenzi ni wa miezi kumi na nane na unatarajiwa kukamilika Oktoba 2024. Urefu wa njia ya kurukia ndege unatarajiwa kuongezeka kutoka mita 1560 mpaka mita 1750 na upana kubakia mita 30 kama ilivyokuwa awali. Gharama ya Mkataba wa kazi hiyo ni shilingi Bilioni 55.9 .
Aidha Mhe. Prof. Mbarawa amewaagiza Tanroads na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kumsimamia Mkandarasi ili kazi ifanyike kwa ufanisi huku akiwaomba wananchi kutoa ushirikano unaohitajika.
Akitoa salamu za Mkoa wa Rukwa Mhe. Queen Cuthbert Sendiga amempongeza, kumshukuru na kumkaribisha Mhe. Prof. Mbarawa Mkoani Rukwa. Ametumia nafasi hiyo kueleza kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya awamu ya Sita katika kipindi cha miaka miwili.
Wakitoa shukrani zao kwa Serikali kwa niaba ya wananchi wa Sumbawanga, Mbunge wa Sumbawanga Mjini na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga wamewaomba na kuwasihi wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan huku wakiendelea kuwaombea viongozi wote wa Serikali ili waweze kuwatumikia bila kuchoka.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa