RC SENDIGA: BILIONI 29 KUBORESHA BARABARA ZA TARURA NA TANROAD
Na. OMM Rukwa
Serikali katika mwaka wa fedha 2022/23 itatumia shilingi Bilioni 29.43 kwa ajili ya kazi za matengenezo na madaraja kwa Wakala wa Barabara (TANROAD) na TARURA kwa mkoa wa Rukwa ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga amebainisha hayo leo (11.10.2022) mjini Sumbawanga wakati Akifungua kikao cha 41 cha Bodi ya Barabara cha kwanza kwa mwaka 2022/2023 ambapo ametoa wito kwa wananchi kutunza miundombinu hiyo.
Sendiga aliongeza kusema kati ya fedha hizo Bilioni 29.43 tayari hadi kufikiwa Septemba 2022, TANROAD imepokea shilingi Bilioni 16.65 na TARURA imepokea shilingi Bilioni 12.78 na kuwa kazi za ujenzi na ukarabati zinaendelea.
Taarifa ya mkoa inaonesha kuwa katika mwaka wa fedha 2021/22 hadi kufikiwa Juni 2022 wakala zote mbili zilipokea jumla ya shilingi Bilioni 27.56 kwa ajili ya kazi za matengenezo ya barabara.
“Ni imani yangu kuwa fedha hizi zilizotolewa kwa ajili ya matengenezo ya barabara katika mkoa wetu wa Rukwa zitawanufaisha wananchi wote, wakandarasi wakubwa na wadogo na vikundi vya akina mama kwa kuwapa kazi za mikono ili kukuza kipato cha kaya” alisisitiza Sendiga.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa agizo la Rais pamoja na agizo la Katibu Mkuu wa CCM la kupunguza matuta kwenye barabara ya Tunduma –Sumbawanga, Katibu Tawala Msaidizi wa Miundombinu, Mhandisi Daudi Sebyiga alieleza kuwa TANROAD imetenga fedha na kuwa kazi ya kumtafuta mzabuni kwa ajili ya kazi hiyo imeanza Septemba 2022.
Katika hatua nyingine Mwakilishi wa Meneja wa TANROAD Mkoa wa Rukwa Mhandisi Suzana Lucas alisema hadi Septemba 2022 hali ya barabara kuu za lami asilimia 76 sawa na ambazo ni kilometa 226 ni nzuri, na zile cha changarawe asilimia 24.68 sawa na kilometa 29 ni nzuri .
Aidha, Mhandisi Suzana aliongeza kusema asilimia 92 ya barabara za mkoa zenye lami sawa na kilometa 70 ni nzuri huku kilometa 645 za changarawe sawa na asilimia 85 ni za wastani na zinapitika wakati wote wa mwaka.
Nae Meneja wa TARURA mkoa wa Rukwa Mhandisi Samson Kalesi alisema hadi kufikia Juni 30, 2022, mkoa ulikuwa umeingia mikataba 49 na wakandarasi yenye jumla ya shilingi 11,288,000,000.00 kwa ajili ya kutekeleza kazi mbalimbali za ujenzi na matengenezo ya barabara, madaraja na makalavati.
Mwisho.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa