Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa Sumbawanga imezinduliwa rasmi leo, Novemba 28, 2025 katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sumbawanga.

Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi, mgeni rasmi, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Bw. Marwa Wankyo ametoa wito kwa bodi hiyo mpya kufanya kazi kwa bidii, uwazi na kwa ushirikiano wa karibu na menejimenti ya hospitali ili kuboresha huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa. Wajumbe wapya wa bodi hiyo wamehimizwa kuchambua kwa kina changamoto zinazoikabili hospitali na kuandaa mwelekeo mahsusi wa maboresho katika maeneo yote ya utoaji huduma.
Aidha, uwepo wa wataalamu kutoka kada mbalimbali ndani ya bodi hiyo umeelezwa kuwa msingi muhimu wa kuleta mabadiliko chanya yanayotarajiwa na jamii. Awali, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Sumbawanga, Dkt. Ismail Macha, aliishukuru Serikali kwa kuunda bodi hiyo, akibainisha kuwa itaimarisha uwezo wa hospitali katika kushughulikia changamoto ili kuongeza ubora wa huduma. Amesema bodi hiyo itakuwa chachu ya kuongeza ufanisi katika usimamizi wa hospitali.

Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Afya, Dkt. Fadhil Kibaya ameipongeza bodi mpya na kuwataka wajumbe kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia miongozo, weledi na dhamana waliyopewa. Ameeleza kuwa ushirikiano kati ya bodi, menejimenti na watumishi wa hospitali ni sharti muhimu katika kufanikisha utoaji wa huduma bora. Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dkt. Ibrahim Mwita, amewataka wajumbe kutumia utaalamu wao kuleta matokeo yenye tija katika utatuzi wa changamoto zinazoikabili hospitali. Amesisitiza kuwa Serikali ina imani kubwa na bodi kutokana na uwakilishi mpana wa taaluma mbalimbali.

Uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa Sumbawanga unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa yatakayoongeza ufanisi, kuimarisha usimamizi na kuboresha huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa