WATOTO 217,674 RUKWA KUPATA CHANJO YA POLIO
Na. OMM Rukwa
Mkoa wa Rukwa umezindua zoezi la utoaji chanjo ya polio kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ambapo imelenga kuwafikia watoto 217,674 katika wilaya za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo.
Mkuu wa Mkoa huo Joseph Mkirikiti leo (18.05.2022) amezindua kampeni hiyo katika kituo cha afya Mazwi kilichopo Manispaa ya Sumbawanga na kutoa rai kwa wazazi kuwapeleka watoto kupata chanjo hiyo ambayo itawakinga dhidi ya ugonjwa wa kupoza.
“Wazazi jitokezeni kupeleka watoto kwenye vituo vya afya ili wapate chanjo hii ya polio ambayo ni salama na itawakinga dhidi ya ugonjwa wa kupoza. Madhara ya polio ni hatari, hivyo tuwalinde watoto wetu ili waendelee kuwa salama” alisema Mkirikiti.
Mkirikiti alieleza kuwa wazazi wawe mabalozi kwa wenzao wenye watoto chini ya miaka mitano kuhamasisha washiriki zoezi hilo ambalo linafanyika kote katika vituo vya afya mkoani Rukwa.
Akitoa taarifa ya kampeni hiyo kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa, Mratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto mkoa wa Rukwa Asha Izina alisema mkoa umepanga kuchanja watoto walio na umri chini ya miaka mitano wapatao 217,674 kutoka katika halmashauri nne za Rukwa.
Mratibu huyo aliongeza kusema maandalizi yamekamilika ambapo tayari watoa huduma 504 watakaoshiriki zoezi la uchanjaji wametakiwa mafunzo na kuwa mkoa umepokea chanjo dozi 250,320 na vifaa vingine.
Naye Mganga Mkuu wa Manispaa ya Sumbawanga Dkt. Sebastian Siwale alisema polio ni ugonjwa unaosababisha watoto kupoza hivyo akitoa wito kwa wazazi na walezi kuwapeleka watoto kwenye vituo vya afya kupata chanjo hii muhimu.
Dkt. Siwale aliwatoa hofu wazazi kuwa chanjo hii haina madhara kwani imekuwa ikitolewa siku zote kwenye kliniki kwa watoto lakini kutokana na nchi jirani ya Malawi kuwa na mlipuko wa ugonjwa huu, Serikali imelazimika kuendesha kampeni hii ili kuwafikia watoto wengi zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari mmoja wa wazazi aliyejitokeza kwenye zoezi hilo Bahati Juma mkazi wa Sumbawanga alisema baada ya kusikia matangazo kwenye redio ndipo akaamua kumpeleka mtoto wake ili apate chanjo ya polio ili asije ambukizwa ugonjwa huo.
Kampeni ya polio imeanza leo na itachukua muda wa siku nne hadi tarehe 21 Mei mwaka huu itakapohitimishwa katika halmashauri za Sumbawanga Manispaa, Sumbawanga vijijini, Kalambo na Nkasi,
Mwisho.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa