Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Julius Kiondo ameahidi kuanza kwa chuo cha ufundi VETA katika Kijiji cha Paramawe Wilayani Nkasi mwezi januari mwaka 2018 baada ya kumaliza vipimo na kupata hati ya majengo hatu itakayomalizwa Desemba mwaka huu.
Majengo yatakayotumika kwaajili ya chuo hicho yalikuwa kambi ya kampuni ya ujenzi wa barabara China Hunan iliyojenga barabara ya Kanazi - Kizi wilayani Nkasi, yenye urefu wa Kilometa 84, majengo ambayo yamejengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 50 na kupitishwa na baraza la madiwani la Halmashauri hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewasisitiza walinzi kuhakikisha wanayalinda majengo hayo ili yasifanyiwe hujuma na kumuagiza mkurugenzi huyo kuhakikisha Kijiji hicho kinakuwa na Zahanati na huduma muhimu za kijamii ili wanafunzi wataoanza kusoma hapo wasipate tabu.
Kijiji hicho ambacho ndio makao makuu ya kata ya paramawe hadi sasa kina jengo la zahanati ambalo linahitaji shilingi milioni 10 kuweza kumaliziwa hivyo mkurugenzi mtendaji ameahidi kuwa karibu na ujenzi huo ili ukamilike kwa wakati maana kwa sasa ili mwananchi apate huduma ya afya ni lazima kusafiri kwa umbali wa kilomita 9 hadi 12.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa