Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda amewaonya wale wote wanaowatia hofu wananchi wa mwambao wa ziwa Tanganyika juu ya ugumu wa maisha baada ya kufanyika oparesheni ya kukamata wavuvi haramu katika mwambao huo.
“kuna kikundi kidogo cha watu kazi yao kuwajaza wananchi hofu, baada ya suala la (operesheni ya) Samaki kuanza tulipokea kama simu sita saba hivi wengine wakitoka hapa kirando, tukafuatilia, tukawaita wale maafisa wanaofanya oparesheni, tukakaa nao, tulikuwa tunaambiwa huruhusiwi hata kusafirisha samaki hata kama ni mmoja, tukajua hali ni mbaya, tuliuliza nia ya operesheni tukaambiwa ni kudhibiti uvuvi haramu sio kuzui biashara ya samaki,” Alisema.
Ameyasema hayo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wavuvi hao walizozielekeza kwa Mkuu wa Mkoa akiwa ziara fupi kata ya kirando ili kujionea maafa yaliyotokea siku chache zilizopita yalisababishwa na mvua kali na kuharibu nyumba 27 na kutia hasara ya shilingi milioni 26.
Ameongeza kuwa wavuvi hao walikuwa wanalalamika kutozwa kuanzia milioni tano kama faini ya kukiuka sheria za uvuvi lakini baada ya mkuu wa Wilaya huyo kutangaza aliyetozwa kiasi hicho ajitokeze ili arudishiwe fedha yake, hakutokea hata mwananchi mmoja.
Aliwataka watu kuacha hofu na wengine kuacha kuwapa wenzao hofu kwa kuwaambia kuwa shughuli za uvuvi hivi sasa hakuna na kwamba watu wanaotegemea shughuli hizo watalala na njaa jambo ambalo si la kweli.
Mmoja wa wavuvi hao Ali Seif alisema kuwa wavuvi wamekuwa wakitozwa faini kubwa kuliko kawaida ikiwemo faini ya shilingi milioni tano na milioni kumi huku mvuvi mwingine Rashid Huseni aliongeza kuwa wakazi wa Kijiji cha Kirando kwa asilimia 99 wanategemea ziwa Tanganyika kwaajili ya vipato vya vya kuendesha maisha hivyo operesheni hiyo inawakosesha vipato hivyo na kusababisha watu wajiingize kwenye uhalifu.
Akitoa maelekezo ya Serikali katika utekelezaji wa zoezi hilo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alisisitiza kuwa aliapa kuitetea na kuilinda sheria ya nchi na hana mpango wa kwenda kinyume na sheria ambayo ilishapitishwa ila ataendelea kusisitiza utekelezaji wake hadi hapo itakapobadilishwa na vyombo husika.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa