Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda ameisisitiza idara ya maendeleo ya jamii wanaoshughulikia usambazaji wa elimu ya Ukimwi katika Mkoa na Halmashauri kuhakikisha elimu ya UKIMWI inawafikia watu wa makundi yote hadi katika ngazi ya vitongoji.
Amesema kuwa wananchi wa vijijini ndio wenye kuihitajia zaidi elimu hiyo kuliko wa mjini ambapo kuna utitiri wa vyombo vya habari na ofisi nyingi zinazoshughulika na kutoa huduma hiyo kuliko vijijini ambapo upatikanaji wa taarifa na elimu hiyo ni changamoto.
“Niataendelea kuwasisitiza watu wa maendeleo ya jamii wakishirikiana na masirika mbalimbali yanayotoa elimu ya UKIMWI kuhakikisha kuwa wanawafikia wananchi wa vijijini, kwani hadi hii leo kuna watu huko vijijini hawajui matumizi ya kondomu na matokeo yake kondomu hiyo moja inatumika zaidi ya mara mbili, mtu anifua na kuitumia tena,” Mh. Mtanda alisisitiza
Ameyasema hayo katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika Kimkoa katika Viwanja vya shule ya Msingi Ndua, Kizwite, Manispaa ya Sumbawanga aliyemuwakilisha mgeni rasmi wa maadhimisho hayo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.
Aidha amewatahadharisha wananchi kuwa kupata UKIMWI haina maana kuwa ni marehemu mtarajiwa bali yeyote atakayeupata ugonjwa huo azingatie ushauri wa wataalamu na kufuata masharti ili aweze kuendelea kuishi na kusaidia kujenga taifa letu.
Kwa upande wake Deo Crispin Mlori aliyeishi na UKIMWI kwa miaka 27 amesema kuwa kwa kufuata masharti wamekuwa wakiishi vizuri yeye na mke wake ambao hadi hivi sasa wana watoto wanne wanaowasomesha kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu.
Awali akisoma risala afisa maendeleo ya jamii Mkoa Aziza Kaliatila amesema kuwa kiwango cha maambukizi kwa mkoa wa Rukwa ni asilimia 6.2, kiwango ambacho kipo juu ya maambukizi ya UKIMWI kitaifa.
“Jumla ya wananchi 308727 wamejitokeza kupima VVU ikiwa wanawake 167623 na wanaume 141104 kwa mwaka2016/2017. Waliokutwa na maambukizi ni 4620 Wanawake 2602 Wanaume 2018.” Aziza alifafanua.
Ameongeza kuwa Mkoa umekuwa ukifanya uhamasishaji wa mapambano dhidi ya UKIMWI kwa kutumia gari la sinema Jumla ya vijiji 89 na Kata 36 zimefikiwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
“Mkoa pia umeendelea kutoa misaada ya kibinadamu kwa vikundi WAVIU vya 34 kwa gharama ya Shilingi 43,000,000 na watoto yatima wapatao 611 wamelipiwa ada za shule jumla ya Shilingi 24,070,000.” Amesema.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa