Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule ameeleza mikakati yake ya kufanya ziara wilaya nzima yenye kata 48 kwa lengo la kukitangaza Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kinacheondelea kujengwa katika Manispaa ya Sumbawanga kwa lengo la kuwaweka tayari wazazi na wanafunzi watakaokuwa na sifa ya kujiunga na chuo hicho.
Amesema kuwa anataka chuo hicho kiwafaidishe wazawa wa Mkoa wa Rukwa kwasabau chuo hicho kitatumiwa na vijana kutoka katika mikoa mbalimbali hivyo ni vyema vijana wazawa wakapata elimu na kuweza kuusaidia Mkoa kufikia lengo la Tanzania ya viwanda hadi ifikapo mwaka 2025.
Pia katika kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa Dkt. Haule amekubaliana na Mstahiki Meya pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kuwa ajenda ya Chuo cha VETA iwe ni ya kudumu kwenye vikao vyao vya madiwani
“Hatutaki tena watu wabebe mageti kutoka Ilemba wayalete hapa mjini, watengenezee kule kule na pia fursa za viwanda kwa mafundi wa mashine za kukobolea mpunga wapate amfunzo hapa na kuweza kutumia ujuzi kule vijijini,” Alisema.
Ameyasema hayo wakati wa ziara ya kujua maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho akiwa na Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo pamoja na wataalamu wengine kutoka katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga wakiongozwa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo pamoja na Mstahiki Meya.
Kwa upande wake Mh. Wangabo alitoa msisitizo kwa wanafunzi juu ya kuzingatia masomo ya sayansi ambayo ndio kipaumbele cha elimu nyingi za ufundi zitakazoanzishwa katika Chuo hicho cha VETA.
“Nitoe rai pia kwa upande wa wanafunzi wenyewe, ili uje kusoma kwenye chuo hiki, fursa ipo kwa wale wanafunzi wa masomo ya sayansi, kwasababu ufundi unaendana na masomo ya sayansi na hisabati, basi wanafunzi watilie umuhimu sana masomo ya sayansi, kwasababu haya ndio yanayotupeleka katika uchumi wa kati wa viwanda,”Alisema
Ujenzi ukikamilika chuo kitaweza kuchukua wanafunzi 900 wa kozi ndefu na 600 wa kozi fupi hivyo, kitakuwa na uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 1,500.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa