Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Halfan Haule ameushukuru mfuko wa penshehi wa PSPF kwa kutoa msaada wa mashuka 50 katika hospitali ya MKoa wa Rukwa na kuushauri kutafuta mahaitaji mengine ambayo hospitali hiyo inahitaji ili kuweza kuboresha huduma katika hospitali hiyo.
Dk. Haule ametoa shukrani hizo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen katika makabidhiano ya mashuka hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa hospitali ya Mkoa muda mfupi baada ya makabidhiano.
“Tunatoa shukrani kwa Mfuko wa pensheni wa PSPF kwasababu mfuko umetekeleza jukumu lake la kimsingi kwa kuisaidia jamii mahitaji ya msingi, na ni motisha mojawapo kwa wafanyakazi wa hospitali ya Mkoa ambao wote wapo kwenye mfuko huu lakini pia kwa watumishi wote wa serikali kwa kuwamini kuwa mafao yao yapo katia mikono salama,” Dk. Haule alisema.
Pia Dk. Haule aliupongeza uongozi wa hospitali ya Mkoa kwa kwa utendaji wao mzuri wa majukumu mbalimbali na kuongeza kuwa tangu ateuliwe na Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga miezi sita iliyopita amepokea malalamiko matatu tu, na yalishughulikiwa yakaisha.
Nae Meneja mafao wa PSPF, Amin Laban alimuhakikishia Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga kuwa kadiri watakavyokuwa wanapata wanachama zaidi nao wataongeza misaada zaidi katika hospitali hiyo.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa