Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule amewaonya kinamama wenye tabia ya kuwanywesha watoto wachanga pombe pindi waliapo kwa lengo la kuwanyamazisha walale ili wao waendelee na shughuli nyiungine za kujitafutia kipato.
Amesema kuwa mambo hayo mara nyingi hujitokeza kipindi cha msimu wa kilimo ambapo mama huenda na mwanawe shambani na pindi anapolia humnywesha mtoto huyo pombe ili apate kuendelea kulima bila ya bughudha yoyote.
“Kwenye mazingira yetu tumeshuhudia watoto wanalishwa vyakula vya ziada lakini hasa pombe, wakati wa masika tumeshuhudia akinamama wanashughuli nyingi za kilimo na kutokana na hizo shughuli hawapati nafasi ya kuandaa chakula cha watoto, na kwavile wanatakiwa kulima basi wanakwenda na pombe shambani, uwongo…kweli? Mtoto akipiga kelele akitaka kunyonya, unamtandika pombe analala chini ya mwembe, hiyo haikubaliki,” Alisisitiza.
Ameongeza Aslimia 19 ya watoto wenye umri chini ya miezi sita wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila ya kupewa kinywaji ama chakula kingine kama inavyoshauriwa na wataalamu ikiwa na maana kuwa asilimia 81 ya watoto wenye umri huo hawanyonyeshwi ipasavyo na kuchanganyiwa chakula hivyo kuwaweka katika hatari ya utapiamlo na magonjwa yanayopatikana katika utaratibu usiofaa.
Ameyasema hayo alipokuwa akizindua wiki ya unyonyeshaji akimuwakilisha mgeni rasmi wa uzinduzi huo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, shughuli iliyofanyika kimkoa katika viwanja vya shule ya msingi Mkomanye, kijiji cha Muze, Wilayani Sumbawanga.
Mmoja wa akinamama waliohudhuria kwenye uzinduzi huo Kalista Mpasa laisema kuwa miongoni mwa sababu zinazosababisha wanawake kushindwa kuwanyonyesha watoto wao kwa muda unaotakiwa ni kutokana na tabia za uasherati na hatimae watoto hao kupata udumavu na kuipa serikali mzigo wa kuwalea.
Nae Efrozina Luheka mama mwenye kitoto kichanga amesema kuwa anaunga mkono serikali kwa kufanya juhudi za kuhakikisha wanawaelimisha kinamama juu ya umuhimu wa kuwanyonyesha watoto na hatimae kuwa na afya njema kuwajali na kupunguza wimbi la watoto wa mtaani.
Kwa upande wake meneja wa mradi wa uzazi salama mkoa wa Rukwa unaofadhiliwa na Global Affairs Canada Dkt. Noah Mwaipyana ameeleza sababu kadhaa wanazozitumia kinamama kukwepa kuwanyonyesha watoto kwa muda unaotakiwa hukunakisisitiza elimu kusambazwa zaidi.
“Kuna sababu nyingi ambazo kinamama wanazitumia kukwepa kunyonyesha watoto, mojawapo ni kuwa na shughuli nyingi na wengine wakisema kuwa maziwa hayatoki na wakati mwingine ni kukosekana kwa uelewa, mtoto akilia wakati mwingine wanachukulia kwamba maziwa hayatoshi na wanakwepa kunyonyesha, sisi tunaingilia kati ili kuhakikisha kwamba mama akishajifungua anapata lisha ya kutosha,” Alisema Dkt. Mwaipyana.
Kwa Mkoa wa Rukwa asilimia 33 tu ya watoto wenye umri wa kuanzia miezi 6 hadi 21 wanapewa vyakula vya mchanganyiko vinavyokidhi mahitaji ya lishe na asilimia 67 ya umri huo wanapewa umlo usiokamilika, na asilimia 12 tu wenye umri wa miezi 6 hadi 23 wanapata chakula cha kiwango cha chini cha ulishaji kama inavyoshauriwa na wataalamu wetu.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa