Rukwa Regional Commissioner Hon. Joachim Wangabo has instructed the four councils in Rukwa to make sure they reach the target of planting 1.5 million tree by the end of the year 2017/2018 so that to reach the target of the region of planting 6 million trees and failure to do so, a council will pay a Million to the winning Council.
Amesema kuwa Halmashauri itakayoshindwa kufikia lengo itatakiwa kulipa faini ya shilingi Milioni 1 kuilipa Halmashauri itakayofika lengo ambapo Halmashauri Mshindi inategemewa kupata shilingi Milioni 3 na fedha hizo itapewa taasisi itakayopanda miti mingi kuliko taasisi nyingine ya serikali ndani ya Halmashauri iliyoshinda hasa mashule ili kuwafundisha wanafunzi umuhimu wa kupanda miti.
“Halmashauri ambayo haikufikia lengo imuume kutoa shilingi Milioni 1 kumlipa mwenzake, katika hizo Halmashauri 4, kwa maana mshindi atapata shilingi Milioni 3, lakini endapo Halmashauri zote zitafikia malengo nitazipa Halmashauri Shilingi Milioni 1, na hiyo fedha itakwenda kwenye taasisi iliyopanda miti mingi kuliko taasisi nyingine hasa mashule,” Mh. Wangabo alibainisha.
Ameongeza kuwa mwaka ujao wa 2018/2019 halmashauri itakayoshindwa kufikia lengo la kupanda miti Milioni 1.5 italipa faini ya shilingi Milioni 5 ili kila halmashauri iweze kufikia lengo na kutimiza maelekezo ya serikali na kuwaonya wote wenye tabia ya kuchoma misitu jambo linalokwamisha jitihada za kutunza mazingira.
Ameyasema hayo alipokuwa akizindua siku ya kupanda miti Kimkoa tarehe 19.1.2018 iliyofanyika katika katika Shule ya Sekondari Matai, Wilaya ya kalambo ambapo miti 100 ilipandwa katika uwanja uliopewa jina la Msitu wa Wangabo kama kuunga mkono juhudi za Mh. Joachim Wangabo katika kuhakikisha kuwa Mkoa wa Rukwa haubaki kuwa jangwa hasa kwa kilimo kinachotegemea mvua.
Nae akisoma risala Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Julieth Binyura kabla ya kumkaribisha Mh. Wangabo alisema kuwa miongoni mwa mikakakti iliyowekwa na Wilaya hiyo ni kuhakikisha kila Kaya inapanda miti mitano na kuhakikisha kila shule inatenga eneo la kupanda miti ya matunda na mbao.
Pia alitumia nafasi hiyo kutoa takwimu za miti iliyopandwa na Wilaya hiyo, “kwa mwaka 2016/2017 miti 497,896 ilipandwa na kwa mwaka 2017/2018 mategemeo ya Wilaya ni kupanda miti Milioni 1.5 pamoja na changamoto za mifugo pamoja na wananchi kukosa hamasa ya kupanda miti tutahakikisha tunatoa elimu na kutenga bajeti kwaajili ya shughuli hiyo,” Alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule amesema kuwa mkakati wa Wilaya ni kuhakikisha kila mwanafunzi kwa shule za msingi na sekondari anapatiwa mti na uongozi wa shule autunze na ukivunwa asilimia 40 atapewa mwanafunzi na asilimia 60 itabaki shuleni.
Nazo taasisi mbalimbali za utunzaji wa mazingira wameahidi kushirikiana na Halmashauri katika kutoa elimu na kuwa na vijiji vya mfano ambavyo wanakijiji wanaweza kutoa ushuhuda juu ya elimu ya mti waliyoipata na faida mabazo zimepatikana kutokana na wingi wa miti watakayokuwa nayo katika vijiji.
Kwa mwaka 2016/2017 Mkoa wa Rukwa ulipanda miti 2,489,296 ambayo ni sawa na asilimia 41.5 ya lengo na mwaka 2017/2018 hadi sasa Mkoa umepanda miti 2,173,649 ambayo ni sawa na asilimia 36.22.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa