Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga imetakiwa kuongeza wigo wa mapato kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kupunguza utegemezi kwa vyanzo vichache vilivyopo ambavyo pamoja na kuwa mapato yake yanakusanywa kwa asilimia 100 bado Halmashauri ina mzigo mkubwa wa madeni ya watumishi na wazabuni.
Hayo yameelezwa leo tarehe 13 Juni 2023 na Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa aliposhiriki Kikao cha Baraza la Madiwani cha kupitia na kujadili taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2021/2022.
Ameeleza kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga imepata hati yenye mashaka kwa sababu mbalimbali ikiwemo mapungufu makubwa katika taarifa ya hesabu za mwisho, mapungufu katika usimamizi wa sheria na taratibu za manunuzi madeni makubwa ya wazabuni na watumishi na kutokamilika kwa wakati kwa miradi ya maendeleo.
Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga imetakiwa kuhakisha miradi yote inakamilika kwa wakati. Miradi hiyo ni pamoja na Kituo Kikuu cha Mabasi Katumba Azimio, Kituo cha Afya Mollo, Shule ya Sekondari Aeshi iliyoko Kata ya Momoka na Hospitali ya Manispaa.
Katika kikao hicho Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ameagiza kuchukuliwa kwa hatua stahiki dhidi ya watumishi wote ambao wameisababishia Halmashauri hoja zilizopelekea kupata hati yenye mashaka.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa