Katika kuhakikisha wananchi wanaelewa utekelezaji wa sera mbalimbali za serikali katika ngazi za mikoa, Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo kupitia Idara ya habari Maelezo inaendesha kipindi cha TUNATEKELEZA kwa ushirikiano na Shirika la Utangazaji Tanzania TBC1.
Katika kufanikisha hilo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amefanikiwa kumaliza kurekodi kipindi hicho na kueleza mikakati mbalimbali iliyofanikiwa na inayoendelea kutekelezwa pamoja na mipango ya baadae katika kuhakikisha kipato cha mwananchi wa mkoa wa Rukwa Kinapanda na hatimae kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Tofauti na ilivyo kawaida Mh.Wangabo alirekodi kipindi hicho katika Shamba la ngano pamoja na alizeti katika Kijiji cha kipande Wilayani Nkasi, akiwa na lengo lakuonyesha mazao mbalimbali yanayolimwa katika mkoa tofauti na zao maarufu la mahindi na mpunga.
Mh. Wangabo amewataka wananchi kufuatilia kipindi hicho ili waone hatua ambayo imefikiwa na mkoa katika kutatua changamoto mbalimbali katika sekta tofauti zinazowalenga wananchi moja kwa moja.
Mahojiano hayo yaliendeshwa na mtangazaji maarufu Eshe Muhidin na kupigwa picha na Mary Hondo na kuongozwa na Elizabeth Shirima.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa