Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Benard Makali amewasisitizia wafanyabiashara wadogo na wakubwa wa mahindi kuachana na tabia ya kusafirisha mahindi kwenda mikoani na badala yake waongeze thamani ya mazao hayo na kusafirisha unga kwenda kwenye mikoa hiyo.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua kikao cha wadau wa uwekezaji kwenye sekta ya Viwanda Mkoani hapa iliyohudhuriwa na wakurugenzi wa Halmashauri, Mameneja kutoka TANROADS, TANESCO, SIDO na wamiliki wa viwanda katika mkoa.
“Mkoa kama wa Dar es Salaama hawahitaji mahindi wanahitaji mazao yanayotokana na mahindi kama ni unga, ama pumba kwaajili ya chakula cha mifugo lakini utaona kuna malori yamejaza magunia ya mahindi yakielekea Dar es salaam badala ya kupeleka unga.” Amesema.
Awali alipokuwa akisoma hotuba kwa niaba ya mkuu wa Mkoa, Benard Makali alisema kuwa Mkoa wa Rukwa unaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kila mwenye nafasi na awezo ashiriki kikamilifu katika kuzalisha bidhaa kwa kuzingatia viwango na ubora wa mahitaji ya Soko.
Aliongeza kuwa Mkoa wa Rukwa una fursa nyingi za uwekezaji katika maeneo ya kilimo, mifugo na uvuvi hiuvyo basi aliwaasa wakurugenzi wa Halmshauri kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa mkoa kujikita katika kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo katika Halmashauri zao ili kuvutia wawekezaji wakubwa na wadogo ili waweze kuwekeza katika sekta hizo.
Kwa mujibu wa orodha ya viwanda Tanzania Bara ya mwaka 2015 kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Mkoa wa Rukwa una takribani viwanda 950 huku viwanda vidogo sana 869 vyenye uwezo wa kuajiri watu kuanzia 1 hadi 4 vikichukua asilimia 91.5, na viwanda vidogo 78 ambavyo ni sawa na asilimia 8.2 ,Viwanda vya kati 2 ambavyo ni sawa na asilimia 0.2 na kiwanda kikubwa 1.
Serikali Mkoani Rukwa imefanya kikao na wadau wa sekta ya viwanda mkoani humo ili kuzungumzia namna ya kuziimarisha fursa zilizopo katika Mkoa na hatimae kuwavutia wawekezaji kutoka mikoani na nje ya nchi kuwekeza katika mkoa Ili kufuikia azma ya serikali ya awamu ya tano ya Tanzania ya Viwanda.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa