Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Rukwa limepatiwa magari matatu mapya ya kisasa kwa lengo la kuimarisha uwezo wake wa kukabiliana na majanga ya moto na kuimarisha huduma za uokoaji.

Uzinduzi wa magari hayo umefanywa na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere leo Oktoba 27, 2025 katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Kupatikana kwa magari hayo kunadhihirisha jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha miundombinu na huduma za dharura nchini.

Serikali imeendelea kuimarisha sekta ya zimamoto na uokoaji kwa kuhakikisha vifaa vya kisasa vinapatikana, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kulinda maisha na mali za wananchi dhidi ya majanga mbalimbali.
Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza kasi na ufanisi katika kutoa huduma za dharura katika maeneo yote ya Mkoa wa Rukwa.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ameelekeza Halmashauri zote za Mkoa wa Rukwa kuhakikisha zinatenga maeneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya kudumu vya zimamoto. Aidha, ameagiza elimu ya kujikinga na majanga ya moto itolewe kwa wananchi kuhusu namna ya kuchukua tahadhari za mapema.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amelitaka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kutumia magari hayo kwa uadilifu na akisisitiza matunzo bora.
Wananchi waliohudhuria uzinduzi huo wameipongeza na kuishukuru Serikali kwa kuiimarisha Zimamoto mkoani Rukwa.
Kupatikana kwa magari mapya ya zimamoto kunatarajiwa kuongeza ufanisi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika Mkoa wa Rukwa, na hivyo kuboresha zaidi huduma za dharura na usalama wa wananchi kwa ujumla.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa