Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Kalambo kwa kufanikisha malengo ya kutatua kadhi ya upungufu wa madarasa kwa kujenga vyumba vya madarasa 20 badala ya sita vilivyokuwa vinahitajika kwaajili ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza watakaochaguliwa katika awamu ya pili Mkoani Rukwa.
Mh. Wangabo alisema kuwa takriban wanafunzi 254 waliachwa katika awamu ya Kwanza ya uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza Wilayani Kalambo ambao ni sawa na mahitaji ya madarasa sita huku kila darasa likitakiwa kubeba wanafunzi 50 na wanne kuwa na darasa la kwao.
“Kila darasa linatakiwa kuwa na wanafunzi 50 vinakuwa vyumba vitano, tano mara 50 ni 250, wanabaki wanafunzi wanne, haw ani lazima wawe na darasa lao, na ndio maana nikasema vyumba sita, lakini halmashauri hii ya Wilaya ya Kalambo, sasa hivi ninavyoongea Pamoja na vyumba vyenu hivi vitano inakamilisha vyumba 20, vyumba 20 ni saw ana utekelezaji wa 333.3%, hii sio mchezo, unaona kuwa vyumba sita ndio vinavyohitajika, unajenga vyumba 20, hii mmejiongeza sana kiasi cha kutatua matatizo yam waka kesho kwa mwaka huu,” Alisisitiza.
Mh. Wangabo ameyasema hayo alipotembelea na kukagua ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa katika shule ya Sekondari ya Mambwe katika kata ya Ulumi, Wilayani Kalambo katika ziara yake ya siku moja ya ukaguzi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa na utengenezaji wa madawati wilayani humo.
Wakati akielezea mipango ya mkoa katika kuyatangaza majina ya wanafunzi hao watakaochaguliwa katika awamu ya pili Afisa Elimu Mkoa wa Rukwa Abel Ntupwa alisema kuwa zoezi hilo la uchaguzi litafanyika kati ya tarehe 5 hadi 10 ya mwezi Februari baada ya kuridhishwa na uwepo wa madarasa ya kutosha wilayani humo Pamoja na kuwarahisishia wazazi kufanya maandalizi ya Watoto wao.
“Tunatoa rai kwa maafisa elimu kata, punde yatakapotoka majina, waende wakahamasishe wanafunzi ili waende shuleni kwa wale watakaochaguliwa awamu ya pili bila ya kukosa hata mmoja, hilo tutalifanya ili kufika tarehe 15 (Februari) ambayo ameisema mheshimiwa Mkuu wa Mkoa au hata kabla ili kuhakikisha wanafunzi wote wameshaingia darasani,” Alisema.
Hata hivyo mh. Wangabo ahkuridhishwa na mwenendo wa ukarabati na ujenzi wa madawati wilayani humo na hivyo kumtaka mkuu wa Wilaya hiyo kuhakikisha wanafunzi hawatakaa chini pindi muhula wa masomo utakapoanza kwa wananfunzi hao watakaochaguliwa katika awamu pili.
Kwa upande wake Mkuu huyo wa Wilaya ya kalambo mh. Carolius Misungwi alisema kuwa kuna mikakati kadhaa amabayo wilaya imejipanga ili kuondoa tatizo hilo la upungufu wa madawati ambapo kwa sasa wanafunzi waliochaguliwa awamu ya kwanza wanahitaji viti na meza 3,528 wakati vilivyopo ni 1,665 na upungufu ni 1863 huku wanafunzi walioripoti wakiwa 1,548 ambao ni sawa na 44.6%.
“Wilaya imeweka mikakati mbalimbali ili wanafunzi wote wanaotarajiwa kujingia kidato cha kwanza wapate viti na meza kama ifuatavyo, kutumia misitu ya shule na halmashauri kuchana mbao kwaajili ya kutengeneza viti na meza, kila shule kutengeneza walau viti 10 kwa kuanzia na kukarabati viti vyote vilivyoharibika miaka mitano iliyopita ili kuondoa uhaba huu kwa kutumia fedha za ukarabati kuongeza samani hizo, kushirikisha jamii kwa kila mzazi kumchangia mtoto wake aliyefaulu kiti na meza katika kuiunga mkono serikali katika juhudi za kutoa elimu bure,” Alimalizia.
Wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao hawajaripoti shuleni hadi kufikia tarehe 26 ni 1921 ambapo wavulana ni 959 na wasichana ni 962 ambao ni saw ana asilimia 55.4 na Wilaya inaanza msako wa wananfunzi hao tarehe 27.1.2021.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa