KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA MKOA WA RUKWA VITA DHIDI YA UKIMWI
Kamati ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI, Kifua Kikuu, Dawa za Kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza imeupongeza mkoa wa Rukwa kwa mafanikio iliyoyapata katika kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI ambapo mkoa una maambukizi ya asilimia 4.4 chini ya kiwango cha kitaifa cha 4.7
Pongezi hizo zimetolewa leo (27.09.2021) na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Fatma Hassan Toufiq (Mb) wakati wa kikao na viongozi na watumishi wa serikali na wadau mjini Sumbawanga.
Akitoa taarifa ya mkoa ,Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu alisema mkoa una watu 34,000 wanaoishi na VVU/UKIMWI ambapo kati yao 28,000 sawa na asilimia 95 wametambuliwa na wanapata huduma za tiba na dawa za kupunguza makali ya VVU
Kuhusu huduma za tohara kwa hiari, Dkt. Kasululu alisema wanaume 34,549 kati ya lengo la watu 35,999 wamepatiwa huduma hiyo kwenye mkoa huo ikiwa ni makakati wa kupungunza maambuzi ya VVU/Ukimwi.
Naye Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma Jaqueline Msongozi (Mb) akizungumza kwenye kikao hicho alitoa rai kwa wanawake kote nchini kutokubali kuwa na mahusiano ya kingono na wananume amabao hawajafanyiwa tohara ili kuondoa hatari ya kupata magonjwa.
" Niwashauri wanawake wenzangu wa Rukwa na kote nchini kabla ya kuwa na mahusiano ni vizuri kujua endapo mwanaume amepata tohara au la .Ukikuta hajapata tohara basi usitoe huduma" alisema Mhe. Msongozi.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Denis Bandisa amesema anashukuru kwa waheshimiwa wabunge hao kupata nafasi ya kutembelea mkoa wa Rukwa kujionea hali ya utoaji huduma za afya kwenye masuala ya UKIMWI na magonjwa mengine.
Bandisa ameihakikishia kamati hiyo kuwa maeleokezo na ushauri watakao utoa wakati wa ziara yao ya siku mbili mkoani Rukwa yatafanyiwa kazi na mrejesho utatolewa kwa Bunge.
Mwisho
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa