Rukwa, 9 Januari 2025
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa Mkoani Rukwa. Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Jastin L. Nyamoga leo tarehe 09 Januari 2025 wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya sekta za afya, elimu, na miundombinu katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mheshimiwa Nyamoga amesema Kamati imeshuhudia kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi katika sekta ya Afya, Elimu na Miundo Mbinu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ambayo inalenga kutatua changamoto za wananchi wa Mkoa wa Rukwa. Amesema kamati imeridhishwa na ubora na thamani ya fedha zilizotolewa katika miradi hiyo.
Naye, Naibu Waziri Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mheshimiwa Zainab Katimba, ameipongeza Kamati ya Bunge kwa kazi nzuri ya ukaguzi wa miradi na kuihakikishia kamati kuwa Serikali itaendelea kupokea maoni, ushauri, na miongozo kutoka kwa Kamati ya Bunge na kuifanyia kazi ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Ziara hiyo ilihusisha ukaguzi wa miradi ya Hospitali ya Wilaya ya Nkasi,ufunguzi wa barabara ya Chala-Ifundwa,ujenzi wa shule mpya ya msingi Kituku, Wilaya ya Nkasi Hospitali ya Manispaa ya Sumbawanga,Barabara ya Malichewe kwa kiwango cha lami ,Shule ya Sekondari Itwelele,Kituo cha Afya Mpui Madaraja Matatu ya Upinde wa Mawe kwenye Barabara ya Laela-Kavifuti
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa