Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Rukwa ikiongozwa na Mheshimiwa Mwenyekti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa, Hajjat Silafu Jumbe Maufi imewataka Wakurugenzi wa Halmashauri Mkoani Rukwa kusimamia vyema miradi ya ujenzi katika maeneo yao.
Kamati hiyo imegiza hayo leo Julai 25, 2024 ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2020-2025 katika Halmashauri za Mkoa wa Rukwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa amesema kuwa ili kupata miradi yenye ubora unaolingana na thamani ya fedha zinazotolewa na Serikali, Wakurugenzi wanatakiwa kuisimamia kwa karibu ikiwemo kuwawezesha wahandisi kuisimamia kwa karibu.
Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere amesema amepokea maelekezo ya Chama cha Mapinduzi na kuahidi kuhakikisha Wakurugenzi wanatekeleza maagizo hayo.
Kamati ya Siasa imekagua miradi 6 yenye thamani ya shilingi Bilioni 23.6 katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. Miradi iliyokaguliwa ni ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Kalumbaleza , ukamilishaji wa vyumba 4 vya madarasa Shule ya Sekondari Mazoka, ukarabati wa barabara ya Ntenzo – Muze – Kilyamatundu, ukamilishaji wa vyumba 4 vya Madarasa Shule ya Sekondari Zimba, Ununuzi wa Boti 2 za doria Ziwa Rukwa na ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Ilemba.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa