Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Maafa, imezishauri Kamati za Usimamizi wa maafa nchini kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa kuwa na mpango wa Kujiandaa na kukabili maafa ili kuwa na uwezo wa utayari wa kujiandaa na kukabili maafa kwa ufanisi.
Akiongea wakati wa mafunzo kwa Kamati ya Usimamizi ya Maafa ya Mkoa wa Rukwa, juu ya Usimamizi wa Maafa kwa Mujibu wa Sheria ya Maafa Na. 7 ya mwaka 2015, Mkurugenzi Msaidizi (Utafiti na Mipango), Ofisi ya Waziri Mkuu, Bashir Taratibu, alifafanua kuwa Mpango huo ni muhimu kwa kuwa huainisha majukumu na hatua zitakazochukuliwa na Kamati za maafa kuanzia ngazi ya kijiji, wilaya na mkoa pamoja na wadau wengine wa maafa.
“Ili kuweza kukabiliana na maafa pindi yanapotokea na kuhakikisha kuwa wanazuia au kupunguza athari za maafa yanapotokea kwa ufanisi tumeishauri kamati ya Usimamizi wa maafa ya mkoa wa Rukwa katika bajeti ijayo watenge bajeti kwa ajili ya maafa, pia wabuni mbinu za upatikanaji wa rasilimali zinazohitajika katika usimamizi wa maafa, hili linawezekana iwapo kamati zote nchini za Usimamizi wa maafa katika ngazi zote zikiwa na Mpango wa kujiandaa na kukabili maafa” alisisitiza Taratibu
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa maafa ya Mkoa wa Rukwa , Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, Winnie Kijazi, aliihakikishia ofisi ya Waziri Mkuu kuwa mkoa huo umeamua kuandaa mpango huo kutokana na changamoto walizo zipata wakati wa maafa ya mvua yenye upepo mkali uliotokea mwishoni mwa mwaka jana katika halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga na Nkasi.
“Tunaishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Maafa kwa uratibu na misaada ya haraka pindi tulipopata maafa , na sisi tumeamua kuwa na ufanisi katika usimamizi wa maafa kwa kuandaa Mpango wa Kujiandaa na Kukabili maafa na tutaelekeza wilaya zote kuandaa mipango yao na kutenga bajeti kwa ajili ya utekelezaji huo” alifafanua Kijazi
Naye Mratibu wa maafa mkoani Rukwa Aziza Kalyatiilya alieleza kuwa, tayari wameandaa Mpango wa kutoa elimu ya Maafa kwa Umma ili kuijengea jamii uwezo wa kujiandaa, kuzuia, au kukabili na kurejesha hali kwa haraka na ufanisi pindi maafa yatakapotokea mkoani humo.
Mnamo mwezi Desemba mwaka jana Halimashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Nkasi mkoani Rukwa zilipatwa na maafa ya mvua yenye upepo mkali iliyosabaisha vifo, uharibifu wa mali na Miundo mbinu. Aidha Kamati ya maafa kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri mkuu, Idara ya Uratibu Maafa, tayari shughuli za kurejesha hali zinaendelea.
Kwa mujibu wa sheria ya Usimamizi wa maafa Na. 7 ya mwaka 2015, inaainisha majukumu ya kamati za usimamizi wa Maafa kuanzia ngazi ya Kijiji hadi mkoa, ambapo kwa mujibu wa sheria hiyo, jukumu la msingi ni kutafuta rasilimali kwa ajili ya usimamizi wa maafa katika ngazi husika, pamoja na Kuratibu na kusimamia shughuli za usimamizi wa maafa na operesheni za dharura ndani ya Kijiji wilaya au mkoa. Pia kutoa taarifa za tahadhari ndani ya eneo husika.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa