Diwani wa kata ya Mtowisa Edgar Malini amepongeza kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo kutimiza ahadi yake ya kutoa kikombe kimoja na mipira mitatu ili kuhamasisha michezo kwa vijana wa kata hiyo na hatimae kujiepusha na kujihusisha na madawa ya kulevya na vitendo vilivyo kinyume na maadili.
Mapema mwezi wa nne mwaka huu Mh. Wangabo alitoa ahadi hiyo alipotembelea miradi mbalimbali ya kimaendeleo katika kata hiyo ambayo inategemewa kujengwa hospitali ya Wilaya ya Sumbawanga na wananchi wake kwa kuipongeza serikali walitoa ekari tatu kwa jeshi la polisi kwaajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi wa jeshi hilo katika ukanda huo wa bonde la ziwa Rukwa.
“Wananchi wa kata yangu wanapenda michezo na kwakweli Mh. Mkuu wa Mkoa alipotoa ahadi ile wananchi kila siku walikuwa wakiniuliza lini mipira itakuja na hicho kikombe, nikawa nawaambia Mh. Mkuu wa Mkoa ni mtu wa kutimiza ahadi zake, hivyo mtulie mipira na kikombe kitakuja na hatimae nimekabidhiwa leo,” Malini alisema.
Mh. Wangabo alikabidhi vifaa hivyo kwa diwani huyo katika ofisi yake mbele ya mtendaji wa Kijiji cha kifinga, kata ya mtowisa na kuahidi kufuatilia maendeleo ya mashindano hayo.
“Vijana ndio nguvu kazi ya taifa letu, wao ndio wa kwanza katika songambele za ujenzi, ulinzi na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo, niliahidi kutoa vifaa hivi na leo hii nimekamilisha ahadi yang una mambo ya uratibishaji wa mashindano hayo nitamuachia diwani ila nitafuatilia maendeleo ya mashindano hayo,” Alisema.
Ameongeza kuwa vijana wanahitaji kuchangamka baada ya kuwajibika katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo na ili kuwaepusha na kujihusisha na kukiuka maadili ni vyema wakajihusisha na michezo ili kuimarisha afya zao na kudumisha umoja na ushirikiano katika maeneo yao wanayoishi.
Tarehe 7.4.2018 ndipo ahadi ilitolewa na vifaa hivyo kutolewa 18.6.2018.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa