Wananchi wa kijiji cha Mayenge kilichopo Kata ya Milepa, Wilayani Sumbawanga wamemstaajabisha Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo baada ya kujenga madarasa manne, nyumba ya mwalimu, vyoo vitatu vyenye jumla ya matundu 16 huku wakibakisha jengo la utawala ili waanze kuwaandikisha wanafunzi na kuanza masomo.
Awali akisoma taarifa mmoja wa mjumbe wa kamati ya ujenzia wa shule hiyo James Kipeta alisema kuwa michango mbalimbali ya vifaa vya ujenzi waliyoipokea pamoja na shilingi milioni 11 fedha taslimu ndio iliyowafikisha katika hatua hiyo na kuongeza kuwa bado kuna ahadi za watu kadhaa bado wanazifuatilia ili kuweza kutia nguvu katika ujenzi huo.
“Pamoja na jitihada zote hizo bado tuna changamoto zifuatazo, madawati, jengo la utawala choo cha kudumu cha nyumba ya mwalimu na mwisho tunakushukuru kwa msaada wako wa mifuko 40 ya saruji uliyotuchangia ulipokuja tarehe 23.8.2018 nayo imetusaidia kufikia hapa.” Alisema
Katika kuhakikisha kasi ya ujenzi huo haisimami Mh. Wangabo aliwaagiza wale wote ambao walitoa ahadi zao za kusaidia vifaa vya ujenzi wa shule hiyo kuhakikisha wanatimiza ahadi zao ndani ya wiki mbili ili wananchi hao waweze kuendelea na ujenzi wa shule hiyo.
Miongoni mwa wadaiwa wa vifaa vya ujenzi wa shule hiyo ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga anayedaiwa mifuko 10 ya saruji , katibu tawala wa mkoa anadaiwa mifuko 15 ya saruji pamoja na Mkuu wa Mkoa mwenyewe anayedaiwa mifuko 10.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa