Nkasi, Rukwa –
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2024, Ndg. Godfrey Mnzava, amewataka Maafisa Lishe mkoani Rukwa kuongeza mkazo wa utoaji wa elimu ya lishe kwa wananchi.
Agizo hilo limetolewa leo Septemba 8, 2024 katika kijiji cha Kantawa, wilayani Nkasi, wakati wa ukaguzi wa shughuli za Maadhimisho ya Siku ya Lishe.
Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 amesisitiza kuwa uhamasishaji wa lishe bora kwa wananchi vijijini ni muhimu ili kupunguza kiwango cha udumavu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Naye Afisa Lishe wa Wilaya ya Nkasi ameeleza kuwa udumavu ni changamoto inayotokana na ukosefu wa uelewa wa kutosha kuhusu lishe bora miongoni mwa wananchi na kwamba Wilaya ya Nkasi imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha elimu inafika kwa wananchi.
Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa takribani nusu ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano mkoani Rukwa wanakabiliwa na tatizo la udumavu huku kiwango cha udumavu kikitajwa kufikia asilimia 49.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 ametoa wito kwa Serikali za Mitaa kushirikiana na maafisa lishe na mashirika mbalimbali kuhakikisha elimu ya lishe inawafikia wananchi kwa ufanisi ili kupunguza tatizo la udumavu.
Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 zimeingia siku yake ya 4 Mkoani Rukwa. Awali Mwenge wa Uhuru ulikimbizwa katika Halmashauri za Wilaya ya Sumbawanga, Kalambo, Manispaa ya Sumbawanga kabla ya kuingia Nkasi.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa