Sumbawanga, 07 Septemba 2024 –
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Godfrey Mnzava, ameihimiza jamii ya Sumbawanga na mkoa wa Rukwa kwa ujumla kuchukua hatua madhubuti za kulinda mazingira kupitia zoezi la upandaji miti. Wito huo umetolewa wakati wa ziara ya Mwenge wa Uhuru katika Msitu wa Hifadhi ya Mbizi, ambapo zaidi ya shilingi milioni 137 zimetumika kuanzisha vitalu vya miti vinavyotarajiwa kutoa miti itakayopandwa na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kuboresha mazingira.
Akizungumza katika eneo la vitalu hivyo, Mhifadhi Mkuu wa Msitu wa Mbizi, Ignas Lupala, alieleza kuwa lengo la mradi huo ni kuwekeza katika uhifadhi wa mazingira kwa kupitia upandaji wa miti unaolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Mradi huo pia unalenga kuwahusisha wananchi wa maeneo jirani kwa manufaa ya kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Godfrey Mnzava, amewataka wananchi wa Rukwa na Tanzania kwa ujumla kutambua umuhimu wa upandaji miti na uhifadhi wa mazingira. “Kila mmoja wetu ana jukumu la kuhakikisha kuwa mazingira yanatunzwa kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho, na upandaji miti ni njia moja wapo ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” alisema Mnzava.
Wananchi wanaozunguka Msitu wa Mbizi pia wameeleza jinsi wanavyonufaika na msitu huo, wakisisitiza kuwa upandaji miti na utunzaji wa mazingira unatoa fursa za kiuchumi na kijamii kwa jamii nzima.
Jumla ya miradi 11 yenye thamani ya shilingi bilioni 10.8 imekaguliwa ,kuwekewa jiwe la msingi na kuzinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa