Mkandarasi Beijing Construction Engineering Company Ltd ametakiwa kukamilisha kazi ya ujenzi wa kiwanja cha Ndege Sumbawanga kabla au ifikapo Machi 2025.
Maelekezo hayo yametolewa Oktoba 2, 2023 na Naibu Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Godfrey Kasekenya alipofanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi inayosimamiwa na TANROADS Mkoani Rukwa.
Miradi iliyokaguliwa katika ziara hiyo ni pamoja na ujenzi unaoendelea wa kiwanja cha ndege Sumbawanga na miradi ya ujenzi wa barabara za Ntendo- Kizungu na Matai- Kasesya.
Akitoa maelekezo kwa Mkandarasi, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kuwa kiwanja hicho ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya usafiri na uchukuzi na kimesubiriwa kwa muda mrefu na wakazi wa Mkoa wa Rukwa. Amemtaka Mkandarasi kukamilisha kazi zote kwa ubora ndani ya muda wa mkataba.
Maboresho yanayofanyika katika kiwanja cha ndege cha Sumbawanga ni pamoja na ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege (runway) yenye urefu wa Km 1.75, ujenzi wa barabara ya kiungio (taxiway) na ujenzi wa maegesho ya ndege( apron).
Mengine ni ujenzi wa jengo la abiria (terminal building), usimikaji wa mifumo ya taa za kuongozea ndege (airfield ground lighting system) pamoja na alama
(aerodrome signage).
Pamoja na kazi hizo Mkandarasi atafanya ujezi wa uzio wa usalama na barabara za kuzunguka uzio wa uwanja na ujenzi wa jengo la kuongozea ndege( Air Traffic Control Tower).
Akiongea kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Rukwa Mheshimiwa Apolinary Simon Macheta Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Sumbawanga amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutenga fedha kwa ajili ya upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Sumbawanga, akieleza kuwa kitakuwa na manufaa makubwa kwa Mkoa wa Rukwa kwa kuwa kitachochea ukuaji wa uchumi.
Maboresho ya kiwanja hicho cha ndege yatagharimu kiasi cha Tsh Bilioni 55.9
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa