Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA Mkoani Rukwa wamesaini mikataba na wakandarasi 18 wa hapa nchini ili kufanyia matengenezo ya barabara za urefu wa kilometa 241.7 mkoani humo zitakazogharimu shilingi Bilioni 2.8.
Kati ya urefu huo barabara za kiwango cha lami kitakuwa ni km 1, changarawe km 77.91, udongo km 163.8 na kuweka alama za barabarani 123, ambapo pia kuna jumla ya vivuko 66 vitakavyotengenezwa vikiwa ni “drifts” 1 na makalavati ya aina mbalimbali 65.
Katika kutekeleza hilo TARURA ilizingazia kutoa kipaumbele kwa wakandarasi waliomo Mkoani Rukwa, na kati ya wakandarasi 18, 12 ni wakandarasi wa mkoa wa Rukwa ambao wanafanya asilimia 67 ya wakandarasi wote.
Awali akitoa hutuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa Benard Makali ameasa kuwa na ufuatiliaji wa karibu wa kazi zinazofanyika ili zifanyike kwa kiwango kinachokubalika na kuhakikisha malipo yanafanyika kwa wakati ili kuwawezesha wakandarasi kukamilisha kazi kwa wakati.
“Serikali iko macho na haitasita kumchukulia hatua za kinidhamu mtumishi yeyote atakayebainika kuwa ameenda kinyume na matarajio ya serikali hii ya awamu ya Tano na kuuchafua Wakala huu na Serikali kwa ujumla kwa vitendo visivyo vya kimaadili.” Makali alisisitiza.
Pia aliwasisitiza wakandarasi kuhakikisha wanatekeleza kazi hizo kwa kiwango kinachokubalika na kukamilisha kazi hizo kwa wakati kwa mujibu wa mikataba iliyopo.
Kwa upande wake Mwakili wa wakandarasi hao Anyosisye Kiluswa ameihakikishia serikali kuwa watafanya kazi hiyo kwa uweledi ulio mkubwa ili thamani ya fedha inonekane na kukamilisha kazi kwa wakati na kutoa matokea chanya kisha akaomba
“Kwa wenzetu wa TARURA tunaomba ushirikiano isije ikawa wanakuja kutukagua halafu sisi tukawa maadui wao na pale tunapoomba malipo basi yale malipo yaweze kutoka kwa wakati,” Kiluswa alisema.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa