Kongamano la Shirikisho la Machinga Tanzania(SHIUMA) limefanyika katika Ukumbi wa Nazareth Mkoani Rukwa leo tarehe 12 Juni 2024. Lengo la Kongamano hilo ni kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutenga Shilingi Bilioni 18.5 kwa ajili ya mikopo kwa wajasiriamali hao nchi nzima.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Nyakia Ally Chirukile amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere katika kongamano hilo ambalo limeenda sambamba na uzinduzi wa Ofisi ya Umoja wa Machinga Mkoa wa Rukwa iliyoko Mtaa wa Florida Kata ya Katandala, Manispaa ya Sumbawanga na uzinduzi wa Soko jipya la mazao lilipo Mandela.
Akizungumza katika tukio hilo Mheshimiwa Chirukile ameleza kuwa Serikali Mkoani Rukwa imesaini Mkataba wa Soko la Kimataifa la mazao ya nafaka litakalojengwa Mtaa wa Kanondo Manispaa ya Sumbawanga.
Aidha Mheshimiwa Chirukile ameongeza kuwa katika kupanua wigo kwa wafanyabiashara kitaifa na kimataifa Serikali inaendelea na ukarabati wa Kiwanja cha ndege cha Sumbawanga kwa zaidi ya Bilioni 60.1 ambapo pia ameelekeza kujengwa kwa chumba maalum cha uhifadhi ili kuwezesha utunzaji na usafirishaji mbogamboga nje ya Mkoa.
Awali akizungumza kwa niaba ya Umoja wa Machinga na Wajasiriamali Mkoa wa Rukwa Thobias Mgalla ambaye ni Katibu wa umoja huo ametoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mkopo utakaosaidia kuinua uchumi wa wajasiriamali Mkoani hapa.
Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini Mheshimiwa Aeshi Khalfan Hilal, Mheshimiwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Hajjat Silafu Jumbe Maufi na Mwenyekiti wa Shirikisho la Machinga Tanzania Bw. Ernest Matondo Masanja.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa