Serikali imefanikiwa kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na matatizo ya uzazi kutoka 74 Mwaka 2020 hadi kufikia vifo 41 kwa Mwaka 2023 kwa kuimarisha miundombinu ya utoaji huduma ya mama na mtoto Mkoani Rukwa.
Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Bw. Msalika Makungu ameyasema hayo alipokuwa akifungua kikao maalum cha kujadili na kuweka mikakati ya kuzuia vifo vya akina mama vitokanavyo na matatizo ya uzazi na vifo watoto vya watoto wachanga kilichofanyika tarehe 30 hadi 31 Mei 2024 Wilayani Kalambo.
Bw. Msalika Makungu amewataka wahudumu wa afya kutekeleza wajibu wao ipasavyo ili kuzuia vifo vya akina mama na watoto vinavyotokana na changamoto za uzazi.
Ameeleza kuwa suala la vifo vya akina mama na watoto linaathiri jamii nzima na kueleza kuwa moja ya njia za kusaidia ni kuishirikisha jamii yote kwa kuanza na viongozi wa kiroho, viongozi wa kisiasa na watalaam wote ili elimu ya kutosha itolewe kwa wanajamii wote.
Takwimu zinaonesha kuwa vifo vya watoto wa siku 0 hadi 7 Mkoani Rukwa vimepungua kutoka 612 kwa Mwaka 2020 hadi kufikia vifo 365 kwa Mwaka 2023.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa