Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere, ameongoza zoezi la upandaji wa miti 4,565 mkoani Rukwa leo Januari 27, 2026 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi ya Siku ya Kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Zoezi hilo limefanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Kalambo pamoja na maeneo mengine mbalimbali ya Mkoa wa Rukwa yakiwemo Wilaya za Nkasi na Kalambo, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Manispaa ya Sumbawanga, likiwa na lengo la kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mheshimiwa Makongoro Nyerere amesema Mkoa wa Rukwa utaendelea kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kulinda mazingira, huku akiwahimiza wananchi kuhakikisha miti iliyopandwa inatunzwa ili iweze kukua na kutoa manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Zoezi hilo limefanyika kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), viongozi wa Serikali ngazi ya Mkoa, watumishi wa umma katika maeneo yao na wananchi, likibeba ujumbe kuwa utunzaji wa mazingira ni wajibu wa kila mmoja.
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alizaliwa tarehe 27 Januari 1960 na leo ametimiza miaka 66. Katika kuadhimisha kumbukizi ya siku yake ya kuzaliwa, Rais Samia ameshiriki zoezi la upandaji wa miti kama ishara ya dhamira yake ya kulinda mazingira na kuhimiza maendeleo endelevu.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa