Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Bernard Makali ameahidi kusimamia michezo katika Mkoa wa Rukwa na kuhakikisha Mkoa haubaki nyuma katika mashindano mbalimbali ya kitaifa ikiwemo ligi kuu ya soka Tanzania bara
Bernard Makali ambaye pia ni Mwenhyekiti wa baraza la Michezo la Mkoa amesema kuwa michezo yote itasimamiwa kuanzia ngazi ya mtaa, kata na wilaya na kuwashirikisha wadau wote kuanzia mwananchi wa kawaida, madiwani, wabunge na taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali zilizopo katika mkoa ili kusukuma maendeleo ya michezo katika Mkoa.
“Michezo yote itasimamiwa, siyo mpira peke yake, lazima wadau wote washirikishwe katika mkoa ili kukuza michezo katika mkoa wetu, kuna mama hapa amelalamika wanawake hawachezi, lakini kuna chama cha netiboli tumekiwezesha kwenda Dodoma kwenye uchaguzi wao na wamefanikiwa, hivyo wote wanawake kwa wanaume watashiriki kwenye michezo,” Makali alisisitiza
Aliyaongea maneno hayo alipoitisha kikao cha wadau wa michezo wa mkoa kabla ya kukabidhi mipira 100 iliyotolewa na chama cha mpira wa miguu taifa (TFF) kwa vilabu 20 vya watoto vilivyopo katika Mkoa wa Rukwa.
Pia aliviagiza vilabu vyote na viongozi wa vyama mbalimbali vya michezo waliohudhuria kikao hicho kuhakikisha wanawahamasisha wananchi kutekeleza agizo la Makamu wa Rais wa Nchi mama Samia Suluhu la kufanya mazoezi kila jumamosi ya pili ya mwezi ili kuhamasisha michezo pamoja na kuimarisha afya za wanarukwa.
“Mkoa huu hatuhamasishi wananchi kufanya mazoezi katika jumamosi ya pili ya mwezi, sasa naagiza sisi tuliopo ndani hapa tuwahamasishe wananchi huko tunapoishi kufanya mazoezi, na nataka kuona ratiba ya kila kilabu kujua wanapofanyia mazoezi kila siku hna hasa jumamosi ya pili ya mwezi,” Alimalizia.
Katika kikao hicho wadau hao walielezea changamoto mbali mbali za michezo mkoani Rukwa ikiwemo kutokuwa na ushirikiano kati ya chama cah mpira cha Mkoa pamoja na vyama vya mpira vya Wilaya jambo linalopelekea kudhoofisha maendeleo ya mpira katika mkoa.
Akizungumzia migogoro iliyopo katika vyama hivyo na namna wanavyoendelea kuitafutia ufumbuzi Mwenyekiti wa Chama cha mpira wa miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA) Bw. Blas Kiondo amesema kuwa tangu aingie madarakani mwaka 2013 amekuwa akikabiliana na changamoto hiyo na kuahidi kuimaliza kabisa.
Kwa upande wake Afisa michezo wa Mkoa Gabrieli Hokororo ametahadharisha kuwa si vyema kuyafufua makovu na badala yake wadau waungane pamoja ili kupeleka maendeleo ya michezo mbele na hatimae Mkoa wa Rukwa usikike kwenye ramani ya michezo katika taifa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa