VIJANA RUKWA WAANZISHA MIRADI YA LISHE ENDELEVU
Mkoa wa Rukwa licha ya kuwa ni mzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula bado unakabiliwa na tatizo la udumavu unaotokana na lishe duni hivyo serikali na wadau wamebuni miradi ya lishe bora kupitia kilimo na ufugaji.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa mradi wa Lishe Endelevu chini ya Shirika la Save The Children Rukwa Emanuel Magoyo wakati wa ziara ya wajumbe wa Kamati ya Lishe ya Mkoa iliyotembelea mashamba darasa, ufugaji kuku, sungura na samaki kwenye wilaya za Sumbawanga na Nkasi mwishoni mwa wiki hii.
Magoyo alisema mradi umefanikiwa kufundisha vijana zaidi ya 700 na maafisa ugani 187 toka wilaya za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo kutekeleza miradi ya lishe bora hatua inayosaidia kuondoa tatizo la udumavu linaloathiri zaidi watoto wadogo.
“Mradi umefankiwa kutoa mafunzo juu ya lishe bora, teknolojia ya umwagiliaji, kutoa mbegu bora za mazao ya mboga mboga, matunda na vifaranga vya kuku bora na samaki ili vijana na akina mama wanzishe miradi ya lishe bora “alisema Magoyo.
Kamati pia ilitembelea shamba darasa la kijana Morgan Yiskaka wa kijiji cha Milundikwa wilaya ya Nkasi ambaye amefanikiwa kuzalisha aina 12 za mazao ya mboga mboga na ufugaji samaki ikiwa ni mkakati wa kuboresha lishe endelevu kwenye jamii.
Akizungumzia mafanikio aliyoyapata chini ya mradi wa lishe endelevu Yiskaka alisema tangu mwaka 2017 vijana na akina mama wengi wamepata mafunzo ya kilimo bora toka shambani hapo chini ya uratibu wa Save The Children.
“Hapa ninazalisha mazao zaidi ya 12 mchanganyiko ili kuchochea upatikanaji wa lishe bora katika jamii. Sasa nina soko kubwa la mazao ya mboga mboga kutokana na watu wengi kutambua faida zake kwa afya” alisema kijana Yiskaka.
Naye Mratibu wa Lishe Mkoa wa Rukwa Teddy Swallo alisema tafiti za mwaka 2018 za Wizara ya Afya zinaonesha tatizo la udumavu liko takribani asilimia 47 kwa mkoa wa Rukwa hivyo kuhitaji mikakati ya kuliondoa kupitia miradi ya lishe endelevu ikiwemo kilimo cha mboga mboga na ufugaji” alisema Swallo.
Swallo alibainisha kuwa mradi wa lishe endelevu kwenye mkoa wa Rukwa unalenga kuboresha hali ya lishe kwa akina mama wajawazito, watoto wadogo na vijana ili waweze kubadili tabia za ulaji chakula bora.
“Pamoja na kuwa na elimu ya ufugaji au kilimo cha mboga mboga ni budi tukabadili tabia zetu za kula ikiwemo kupata mlo kamili kwa makundi yote matano ya nafaka, wanyama, mboga mboga, matunda na mafuta” alisisitiza Swallo.
Mratibu huyo alitaja madhara ya udumavu kwa watoto kuwa ni pamoja na kuwa na uwezo mdogo wa kufikiri (akili) na kuwa na uwezekano mkubwa wa kupata maradhi mbalimbali.
Akizungumzia juu ya mradi wa ufugaji kuku bora Mkulima Kiongozi wa kijiji cha Mkangale Namanyele Elizabeth Ngalawa alisema wanashauri wakulima wasipige mahindi dawa zisizo na ubora ili kutoathiri chakula cha binadamu na mifugo.
Aliongeza kusema kikundi chao kinajihusisha na ufugaji bora wa kuku aina na Saso pamoja na shamba kilimo ili kujenga tabia ya kula lishe bora ikiwemo kukuza kipato cha kaya baada ya kupata mafunzo toka wataalam wa mradi wa USAID/Lishe Endelevu.
Mwisho.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa