Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaagiza maafisa ugani wote wa mkoani humo kuhakikisha wanawafikia wakulima kwenye mashamba yao na kuwapa elimu ya kukabiliana na wadudu aina ya viwavijeshi vamizi ambao wanaonekana kuanza kuleta athari katika wilaya ya Nkasi.
Amesema kuwa wakulima wengi hawana elimu ya kukabiliana na wadudu hao hasa kujua aina ya dawa ya kutumia ili kuwaua na wasiendelee kuharibu mazao na kuongeza kuwa ni wakati wao sasa maafisa ugani kufanya kazi ya kuwasaidia wananchi kupata matokeo bora ya mavuno kwa kutoa elimu ya kukabiliana na wadudu waharibifu na magonjwa.
“Kitu cha kufanya ni maafisa ugani wote na maafisa kilimo wote washuke kwenda kwenye mashamba, wakague na kutoa ushauri wa moja kwa moja, dawa zipo zinapatikana wanaanzia dawa gani inayofuata ni ipi, ili tuweze kuwasaidia wakulima waweze kuokoa haya mahindi, DC hawa watu wasimamiwe washuke asibaki mtu kwenye ofisi zao,” Alisisitiza.
Ameyasema hayo baada ya kuona athari ya viwavi jeshi alipotembelea shamba la mkulima wa mahindi Alex Ndenge katika ziara yake ya kuangalia maendeleo ya kilimo kwa wakulima na changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo upatikanaji wa pembejeo pamoja na mashambulizi ya wadudu na magonjwa ya mazao Wilayani Nkasi.
Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Mkoa wa Rukwa Ocran Chengula alifafanua namna ya kupambana na wadudu hao na kutoa tahadhari kwa wakulima kuwa na tabia ya kupanda kwa kipindi kimoja na sio kupishana kwani hali hiyo hupelekea wadudu hao kuhama kutoka sehemu moja hadi nyingine ili kufuata mimea teke.
“Kuna sumu nyingine ukipiga inakuwa kwenye mmea, kwasababu huyu (mdudu) anatoa kinyesi kwahiyo ile sumu inaingia kwenye mmea kwahiyo anapokula anapata madhara anakufa, kwahiyo katika hatua za kwanza tunashauri (dawa aina ya) Duduba na hatua ya pili tunashauri dawa inaitwa “systemic” japo zina majina tofauti tofauti ni amjina ya kibiashara ila itumike hiyo baada ya kuona kwamba wameshaanza kutoa huu uchafu” Alieleza.
Kwa mujibu wa Afisa kilimo wa halmashauri ya wilaya ya Nkasi Emanuel Sekwao amesema kuwa viwavijeshi vamizi hao wameshaathiri kwa asilimia 2 mpaka 5 kutegemea eneo lakini bado haijafikia hatua ya wadudu hao kuharibu mimea kiasi cha kushindwa kuzaa.
Katika kipindi cha mwaka 2018/19 mkoa unalenga kulima jumla ya hekta 599,345.45 za mazao mbalimbali, kati ya hizo hekta 517,482.15 ni za mazao ya chakula na hekta 81,863.3 za mazao ya biashara. Kutokana na eneo hilo mkoa unategemea kuzalisha jumla ya tani 1,817,171.84 za mazao ya chakula na biashara. Katika kiasi hicho tani 1,680,701.6 ni za mazao ya chakula na tani 136,470.25 ni za mazao ya biashara.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa