WATENDAJI KATA NA MAAFISA TARAFA SIMAMIENI MAPATO YA HALMASHAURI- RC MKIRIKITI
Maafisa Watendaji wa Kata pamoja na Maafisa Tarafa wa Mkoa wa Rukwa wametakiwa kutambua kuwa wanalo jukumu la kusimamia ukusanyaji na matumizi ya fedha zitokanazo na mapato ya ndani kwenye halmashauri.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ametoa maelekezo hayo leo (28.10.2021) wakati alipofanya mkutano na Maafisa Tarafa wote wa mkoa wa Rukwa na Maafisa Watendaji wa Kata mjini Sumbawanga na kuwasisitiza kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha toka kwa vyanzo mbalimbali.
Aliwataka watendaji pia hao wa kata na tarafa kuelimisha wananchi kujitokeza kupata chanjo ya kinga dhidi ya ugonjwa wa korona na pia kuhamasisha wananchi kujiandaa kwa zoezi la sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwaka 2022.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa chanjo ya UVIKO-19 Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu, aliwataka watendaji hao kuwa mstari wa mbele kwa wao binafsi kuchanja kisha kuhamasisha wale ambao bado hajawachanja.
Dkt. Kasululu aliongeza kusema mkoa umepokea dozi 24,183 za chanjo ya UVIKO-19 awamu ya pili aina ya Sinopharm ambapo kazi ya kuhamasisha wananchi imeanza hivyo amewataka watendaji hao kushiriki kwenye zoezi hilo pamoja na wataalam wa afya kwenye maeneo yao.
Naye Afisa Utumishi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa Sabina Songela akitoa mada kuhusu majukumu na wajibu wa Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata alisema wanalo jukumu la kusimamia suala la upatikanaji huduma kwa wananchi ili kuleta ustawi na amani kwenye maeneo yao.
Mkutano huo wa Maafisa Tarafa toka tarafa zote 19 za Mkoa wa Rukwa na Maafisa Watendaji Kata toka kata 20 za Manispaa ya Sumbawanga ni kwanza tangu Mkuu huyo wa Mkoa alipoteuliwa kuongoza mkoa wa Rukwa hapo mwezi Mei mwaka huu na ulilenga kuwakumbusha wajibu wao kwenye utekelezaji wa majukumu ya serikali.
Mwisho.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa