Rukwa, 19 Mei 2025.
Mapokezi ya Madaktari Bingwa Mkoani Rukwa yamefanyika leo Mei 19, 2025 yakiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Bw. Msalika Robert Makungu.
Madaktari Bingwa 33 wamewasili Mkoani hapa kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa katika hospitali zote za Wilaya za Mkoa wa Rukwa.
Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Bw. Msalika Makungu ameeleza kuwa ujio wa Madaktari Bingwa hao unalenga kusogeza huduma za kibingwa kwa wananchi, ili kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na changamoto za uzazi, kupunguza vifo vya watoto wachanga pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya waliopo kwenye vituo vya afya na hospitali za Wilaya.
Katibu Tawala wa Mkoa amemshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuleta huduma za kibingwa mara kwa mara Mkoani hapa.
Huduma zitakazotolewa na madaktari bingwa hao ni pamoja na huduma za kibingwa za magonjwa ya wanawake, ukunga, huduma za kibingwa za magonjwa ya watoto na watoto wachanga, huduma za kibingwa za upasuaji wa mfumo wa mkojo, huduma za kibingwa za magonjwa ya kinywa na meno na huduma za kibingwa za magonjwa ya ndani.
Bw. Makungu ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma za kibingwa zinazotarajia kutolewa kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 19 hadi 24 Mei 2025 katika Hospitali ya Manispaa ya Sumbawanga, Hospitali ya Wilaya ya Kalambo, Hospitali ya Wilaya ya Nkasi, na Hospitali ya Wilaya ya Sumbawanga.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa