Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa wamemuhakikishia Mkuu wa Mkoa huo Mh. Joachim Wangabo kuwa suala la upungufu wa madarasa ndani ya wilaya hiyo litakuwa historia baada ya kila Diwani asiyekuwa na Shule ya Sekondari katika kata yake kuanza ujenzi wa msingi wa Shule katika kata zao baada ya wanafunzi wengi wanaomaliza shule za msingi kukosa nafasi za kuchaguliwa kuendelea na kidato cha kwanza kutokana na upungufu wa madarasa.
Akizungumza katika Songambele ya ujenzi wa Madarasa tisa ya Shule ya Sekondari Matai iliyopo makao makuu wa Wilaya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mh. Daudi Sichone amesema kuwa madiwani hao wamekubaliana kutolala hadi kuhakikisha wanatekeleza ahadi walizotoa kipindi wanaomba kura wakati wa kampeni za Uchaguzi mkuu ilizofanyika Oktoba, 2020.
“Kwahiyo Mheshimiwa mkuu wa Mkoa nikuahidi kuna zaidi ya kata tano ambazo zinaanza kujenga shule za sekondari katika Wilaya hii ambazo nazijua kabisa kuna (kata za)Lyowa, Mkali, Samazi, kuna Sundu wamekaa vikao jana wamesema wakope tofali waanze, kuna Kata ya Mnamba, hao wako tayari na nina uhakika mwakani hii adha ya mchakamchaka haitakuwepo,” Alisema.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Matai Mh. Vitusi Tenganamba alisema kuwa baada ya agizo la Mkuu wa mkoa huo la kukamilisha vyumba vya madarasa, wananchi wa kata hiyo na kata ya jirani ambao wanafunzi wao wanasoma katika shule hiyo walijitoa kwa nguvu zote huku wao wakiendelea kuwahamasisha kushiriki katika ujenzi huo.
“Naomba muendelee kuwa na moyo huo kama alivyosema Mkuu wa Mkoa ni kwamba majengo haya yanajengwa kwaajili ya manufaa ya Watoto wetu wenyewe, kama mnavyojuwa kuwa Elimu ndio Ufunguo wa Maisha, tukisema tusijitoe kwamba serikali ndio ilete, hamna lazima tujitoe kama tunavyojitoa ili tuweze kupata madarasa,” Alieleza.
Naye Diwani wa kata ya Lyowa Mh. Legius Boimanda ambaye wanafunzi wa kata yake wanategemea kusoma katika Shule ya Sekndari ya Matai alimuomba Mkuu wa Mkoa waungane kuelekeza nguvu katika kata Lyowa ambapo wameanzisha ujenzi wa shule ya Sekondari ili kupunguza adha ya kila mwaka ya wanafunzi kukosa pa kusoma.
“Kwa niaba ya Wanachi wote tunaombeni ushirikiano wananchi wa kata ya Matai na kata ya Mkali tushirikiane kama tulivyofanya hapa kwasababu hii ni faida ya wananchi wetu ambao wanapata adha kutokana na kukosa shule ya kuwapelekeka wanafunzi kusoma baada ya kusema hayo nasema ushirikiano huu udumu na mungu awabariki,” Alimalizia.
Aidha, akitoa ufafanuzi wa nguvu za wananchi wa kata za Matai, Mkali na Lyowa zilizotumika kujenga madarasa hayo Mkuu wa Shule ya Sekondari Matai Jenus Joseph alisema kuwa kulingana na mahesabu ya kitaalamu na BOQ nguvu iliyotumiwa na wananchi thamani yake ni sawa na shilingi milioni 74.
“Kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa uliagiza vyumba saba vijengwe, vyumba saba vinajengwa kwa nguvu za wananchi hadi kufika hatua ya upauaji au usawa wa linta, kuna wananchi wa kata tatu ya Matai, Lyowa na Mkali, wanaoshiriki katika ujenzi huu ambao majengo yao yamefikia usawa wa linta na kutokana na mahesabu ya mafundi ni kwamba ujenzi huu kwa nguvu iliyotumika tulitakiwa kutumia shilingi 74,000,580,” Alisema.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa huo Mh. Joachim Wangabo alitoa pongezi kwa ushirikiano ulioonyeshwa na wananchi hao Pamoja na viongozi wa Wilaya hiyo katika kuhakikisha zoezi la ukamilishaji wa vyumba vya madarasa kwaajili ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza unakwenda kwa kasi na kuahidi kurudi tena baada ya wiki mbili ili kuona ukamilifu wa vyumba hivyo.
“Nilikuja hapa tarehe 24.12.2020 hali ilikuwa mbaya sana na nilikasirika sana, na nilionyesha hisisa zangu za kukasirika na hisia zile za kuakisirika DC alizibeba naye alionesha hisia zake za kukasirika bila ya shaka mliona yalitofuata lakini leo hii kwakweli nimefurahi sana, siku ile ndio tulikuwa tumeanza kuchimba msingi nami nilishiriki kubeba mawe, kulikuwa na vyumba viwili, sasa hivi kunaonekana, kuna vyumba tisa viko hapa, viwili vinamaliziwa na saba viko hatua ya linta, hii ni hatua nzuri ndani ya wiki mbili,”Alieleza.
Mh. Wangabo ametoa pongezi hizo baada ya kuetembelea Shule ya Sekondari Matai inayojenga madarasa tisa huku saba kati ya hayo ni nguvu za Wananchi na mawili yakijengwa kwa fedha za mradi wa EP4R katika Ziara yake ya kukagua shule nne za wilaya hiyo zenye upungufu wa madarasa.
Aidha, Mh. Wangabo amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kalambo kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha Kwanza wanakaa kwenye viti na madawati baada ya kila Shule ya Sekondari wilayani humo kuwa na mpango wake wa kutafuta vifaa hivyo kutokana na Wilaya hiyo kuwa na upungufu wa viti na madawati 2,617 huku mahitaji yakiwa 3,759.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa