Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameisifu mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga kwa kutimiza wajibu wake kisheria kwa kutoa hukumu ya miaka 20 jela kwa waliohusika kwenye kuwakata mikono watu wenye ulemavu wa Ngozi.
Amesema kuwa watu wenye ulemavu wa ngozi na wasio na ulemavu huo watambue kuwa Sheria inawalinda na ni wajibu wa serikali kuhakikisha kuwa wananchi wake wanakuwa salama muda wote na kusisitiza kuwa si kweli kwamba watu wenye ulemavu wa Ngozi hawapewi ulinzi wa kutosha na kwa kupitia kesi hizi wajue kuwa Sheria inawalinda na waendelee kuwa na Imani.
Pia amewaonya wananchi wenye tabia ya kujichukulia sharia mikononi kwa kuwataka kushirikiana na vyombo vinashughulika na kutoa haki nchini kwa kutoa ushahidi pale unapohitajika.
“Kuna wananchi wanapenda kujichukulia sharia mikononi jambo hili halifai cha muhimu ni kuripoti na kama kuna ushahidi unahitajika basi ni jukumu lao kuvisaidia vyombo vya usalama kupata ushahidi huo ili haki itendeke kama ilivyokuwa kwenye hukumu ya kesi hizi , jambo ambalo limepewa kipaumbele ni ushahidi” Amesema.
Pia aliwasifu mawakili wa pande zote mbili kwa kutimiza kazi yao nzuri ya kuhakikisha kwamba haki inapatikana na kuwaomba waendeleze kasi hiyo ya kuzingatia weledi katika majukumu yao.
Aidha alitumia nafasi hiyo Kuiomba mahakama kushughulikia maovu yote isiwe tu ya kesi za wenye ulemavu wa ngozi lakini pia wala rushwa, wabadhirifu wa mali ya umma, wakwepaji wa kulipa kodi.
Hukumu ya Kesi ya Kwanza
Kesi hii namba 1/2015 iliyosomwa na Mheshimiwa Jaji Mkuu Mahakama kuu Kanda ya Sumbawanga Dk. Adam Mambi Ilimhusisha mtoto Mwigulu Magesa Matonange mwenye umri wa miaka 7 aliyevamiwa alipokuwa akichunga ng’ombe na kukatwa kiungo cha mkono wa kushoto na watuhumiwa kutoweka na kiungo hicho katika Kijiji cha Nsia, Tarafa ya Mtowisa, wilayani Sumbawanga Februari 15, 2013
Watuhumiwa hao walitoweka na kiungo hicho na hatimae walikamatwa na polisi Aprili 20, 2013 mkoani Tabora wakiwa katika harakati za kutafuta mnunuzi.
Kesi hiyo ilijumuisha watuhumiwa 10 ambao sita kati yao walikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 kila mmoja na wengine wanne kuachiwa baada ya mahakama kukosa ushahidi wa kutosha wa kuwatia hatiani watuhumiwa hao.
Washtakiwa sita kati ya kumi waliokutwa na hatia ni Ignas Sungura, James Paschal, Ibrahim Tela, Faraja Jailos Mwezimpya, Weda Mashilingi na Nickson Ngalamila. Walioachiwa ni Kulwa Mashilingi, Peter Said Msabato, Hamis Rashid Manyanywa na James Patrick Ngalamila.
Akisoma hukumu hiyo Jaji Dk.Adam Mambi alisema Mahakama imeridhishwa na ushahidi wa kiungo uliotolewa na upande wa mashtaka uliokuwa na mashahidi 12 wakiwamo daktari na mkemia.
Jaji Mambi alisema Mahakama imejielekeza katika mambo kadhaa ya msingi ili kuthibitisha makosa hayo; iliangalia ushahidi wa mazingira; kitendo cha washitakiwa kukutwa na kiungo cha binadamu wakitafuta soko; na nia ovu ya kutenda kosa na kusababisha maumivu makali au kifo.
Alisema kosa la kula njama ya kuua, adhabu yake ni kifungo cha miaka 14 jela kwa kuzingatia kifungu cha Sheria Namba 215 ya kanuni ya adhabu sura 16, huku kosa la kufanya jaribio la kutaka kuua adhabu yake ni kifungo cha maisha jela kwa kuzingatia kifungu cha Sheria Namba 211 ya kanuni ya adhabu sura 16 na kosa la kusababisha ulemavu wa kudumu adahabu yake ni kifungo cha maisha jela kwa kuzingatia kifungu cha Sheria Namba 222 ya Kanuni ya adhabu sura 16.
Hukumu ya Kesi ya Pili
Kesi hii namba 46/2015 iliyosomwa na Mheshimiwa Jaji Mkuu Mahakama kuu Kanda ya Sumbawanga Dk. Adam Mambi ilimhusisha Maria Chambanenge (39) Kijiji cha Mkowe, Miangalua, Wilaya ya Sumbawanga Vijijini, Mkoa wa Rukwa.
Tukio hili lilitokea usiku wa 11/2/2013 chumbani kwake akiwa amelala na wanawe, Maria ni albino na haoni vizuri. Sasa ameongezewa ulemavu wa viungo. Huyu ni mama wa watoto wanne: Shukuru (8), Edron (6), Rahab (3) na Emma (miezi mitano). Mama huyu ni mke wa tatu wa Gabriel Yohana.
Maria alieleza namna ilivyotokea ““Usiku wa manane, kati ya saa saba na saa nane hivi, Nilisikia vishindo vya nyayo vikitokea sebuleni ambako mwanangu Shukuru na Edron walikuwa wamelala. Ghafla nikamwona mume wangu ameshika upanga ananishambulia kichwani. Nikawa nashangaa na kuwaangalia usoni bila kujua kwa nini alikuwa ananishambulia. Akasema, “Nyamaza!” Mimi nikawa nalia. Akasema, Pole! Nyamaza!”
Watuhumiwa walishtakiwa kwa makosa matatu kula njama ya kuua, jaribio la kuua mtoto mlemavu wa ngozi na kumsababishia ulemavu wa kudumu.
Watatu kati ya watuhumiwa 4 wa kesi hiyo ambao ni pamoja na Michael Kazanda na Linus Silikala Selemani walipewa kifungo cha miaka 20 kila mmoja kwa kosa la pili na la tatu na miaka 14 kwa kosa la kwanza.
Ntogwa Cosmas alikutwa na kosa la kwanza la kula njama za mauaji baada ya kushiriki kwa njia ya mawasiliano bila ya kuwepo eneo la tukio na kumsababishia kupewa kifungo cha miaka 14 na Frank Bernard kuachiwa huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuwasilisha ushahidi usiopingika.
Jaji Mambi alisema Mahakama imejielekeza katika mambo kadhaa ya msingi ili kuthibitisha makosa hayo; iliangalia ushahidi wa mazingira; kitendo cha washitakiwa kukutwa na kiungo cha binadamu wakitafuta soko; na nia ovu ya kutenda kosa na kusababisha maumivu makali au kifo.
Alisema kosa la kula njama ya kuua, adhabu yake ni kifungo cha miaka 14 jela kwa kuzingatia kifungu cha Sheria Namba 215 ya kanuni ya adhabu sura 16, huku kosa la kufanya jaribio la kutaka kuua adhabu yake ni kifungo cha maisha jela kwa kuzingatia kifungu cha Sheria Namba 211 ya kanuni ya adhabu sura 16 na kosa la kusababisha ulemavu wa kudumu adahabu yake ni kifungo cha maisha jela kwa kuzingatia kifungu cha Sheria Namba 222 ya Kanuni ya adhabu sura 16.
Hukumu ya Kesi ya 3
Kesi hii namba 39/2016 iliyosomwa na Mheshimiwa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga John Samwel Mgeta ilimhusisha mtoto Baraka Cosmas mwenhye umri wa miaka 6 anayeishi na wazazi wake kijijini Kipeta, Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga ameshambuliwa na kujeruhiwa vibaya kwa kukatwa kiganja cha mkono wake wa kulia.
Tukio hilo la kikatili lilitokea saa saba usiku wa tarehe 12/3/2015 na wakati hayo yakitokea baba mzazi wa mtoto huyo inadaiwa alikuwa amelala katika nyumba ya mkewe mdogo kijijini humo. Na baadaye mtoto huyo alipelekwa kulazwa katika Kituo cha Afya cha Kamsamba wilayani Momba mkoani Mbeya kwa matibabu akiwa pamoja na mama mzazi.
Mama mzazi Prisca Shaaban Mpesya (28), mkazi wa Kitongoji cha Kikonde, Kijiji cha Kaoze katika Kata na Tarafa ya Kipeta wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa, alisema tukio hilo lilimkutana saa saba usiku, wakati akitaka kutoka nje kujisaidia.
“Nilikuwa natoka nje kwenda kujisaidia, sijui ilikuwa saa ngapi kwa sababu sikuwa na saa, nje juu ya mlango tuliweka taa ya Mchina ya solar ambayo ilikuwa inaangaza, hivyo sikuwa na hofu,” akihadithia wakati alipokuwa amelazwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
Anasema ghafla tu alipofika mlangoni akashtuka kuona mtu akija mbio, akaipiga taa na kuivunja, kukawa giza.
“Nikajua huyu hakuwa mwema, hivyo nikajiandaa kupambana naye, alikuwa mwanamume mwenye nguvu kunishinda, lakini nilimdhibiti kwa sababu alitaka kuingia ndani kwa nguvu nami sikutaka kwa sababu wanangu walikuwa wamelala chini angeweza kuwaumiza.
“Mara nikasikia kitu kikinipiga kichwani pa! Nikaanguka na kupoteza fahamu. Nilipozinduka nikamwona mwanangu Baraka analia, kitanga cha mkono kimekatwa.” Akaongeza: “Natamani watu wanaofanya mambo haya wauawe hadharani.”
Anasema, mumewe Cosmas Yoramu Songoloka hakuwepo kwani alikuwa ameaga tangu mchana kwamba anakwenda kilabuni kunywa pombe, na mpaka majira hayo hakujua kama alikuwa kilabuni ama alikwenda kwa mke mdogo ingawa haikuwa zamu yake.
Jitihada za kupata tiba katika kituo cha afya Kamsamba wilayani Sumbawanga zilishindikana, hivyo kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Prisca ni mama wa watoto watatu wenhye ulemavu wa Ngozi na wakati tukio hilo likitokea alikuwa na mimba ya mtoto wa tatu na pia alikuwa na binti mdogo Lucia mwenye umri wa miaka 3 ambaye pia ni mlemavu wa Ngozi. Na Baraka (6) na wa kwanza anaitwa Shukuru (8) ambaye yeye si mlemavu na alimuacha nyumbani na baba yake wakati alipokuwa hospitali ya rufaa Mbeya.
Watuhumiwa wa kesi hiyo ni pamoja na Cosmas Yoram Songoloka (baba wa mtoto) Andius George Songoloka, Unela Shinji Jiloya Seme (anayedaiwa kukiri polisi kwamba ndiye aliyekata kiganja na ndiye aliyewaongoza polisi hadi kumkamata ‘tajiri’ Kalinga), na Mihambo Kanyenga Kamata maarufu kama Bichi (ambaye ni mganga wa jadi) na Sajenti Kalinga (Tajiri aliyetaka kununua kiganja hicho kwa Milioni 100) ambao walikambatwa tangu April mwaka 2015.
Katika kusoma hukumu hiyo Jaji John Mgeta alimuacha huru baba wa mtoto baada ya upande wa mashtaka kuwa ushahidi hafifu wa kumtia hatiani na hivyo kushindwa kuthibitisha bila ya shaka uhusika wake ushahidi kushindwa kumtia hatiani baba huyo
Mnunuzi wa kiungo hicho Sajenti Kalinga alipewa kifungo cha miaka 8 jela kwa kukutwa na kiganja na kukiri kosa tangu mwanzo na pia kutoa ushirikiano kwa vyombo vy a usalama.
Kwa upande wa Andius George Songoloka, alipatikana na hatia ya makosa matatu, kula njama ya kuua – alifungwa miaka 10, jaribio la kuua mtoto mlemavu wa Ngozi – alifungwa miaka 15 na kumsababishia ulemavu wa kudumu- alifungwa miaka 18.
Unela Shinji Jiloya na Miambo Kanyenga Kamata walikutwa na makosa mawili jaribio la kuua mtoto mlemavu wa Ngozi – walifungwa miaka 15 na kumsababishia ulemavu wa kudumu- walifungwa miaka 18. Hatimae kutumikia kifungo cha miaka 18 jela kwa kila mmoja.
Alisema kosa la kula njama ya kuua, adhabu yake ni kifungo cha miaka 14 jela kwa kuzingatia kifungu cha Sheria Namba 215 ya kanuni ya adhabu sura 16, huku kosa la kufanya jaribio la kutaka kuua adhabu yake ni kifungo cha maisha jela kwa kuzingatia kifungu cha Sheria Namba 211 ya kanuni ya adhabu sura 16 na kosa la kusababisha ulemavu wa kudumu adahabu yake ni kifungo cha maisha jela kwa kuzingatia kifungu cha Sheria Namba 222 ya Kanuni ya adhabu sura 16.
Utetezi
Katika kesi zote viungo hivyo vilichochukuliwa kutoka kwa washtakiwa hao kilipelekwa kuchunguzwa vinasaba (DNA) kwa lengo la kuthibitisha iwapo vilikuwa vya waathirika.
Waliokuwa wakitetewa na mawakili wanne ambao ni Bartazar Chambi, Charles Kasuku, Peter Kamyalile na Mathias Budodi
Awali, Wakili wa Serikali Fadhili Mwandoloma aliitaka mahakama kutoa adhabu kali kwa watuhumiwa hao ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaotenda makosa kama hayo.
Nao, mawakili wa upande wa utetezi waliiomba mahakama kupunguza adhabu kwa wateja wao kwa kuwa tayari wamekaa mahabusu kwa zaidi ya miaka minne kitu ambacho ni funzo tosha kwao hivyo hawawezi kurudia kutenda tena makosa hayo.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa