Wakati Wakristo wote duniani wakisheherekea sikukuu ya Pasaka, Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewashauri wakristo wote katika mkoa huo kuhakikisha wanafikiria namna ya kulishana mwili na damu ya bwana katika utekelezaji wa ibada zao ili kujikinga dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona.
Ametoa kauli hiyo baada ya kuona utaratibu uliowekwa katika Kanisa Katoliki Parokia ya Namanyere juu ya utoaji wa sadaka pamoja na kula Ekaristi takatifu kutozingatia tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona kutokana na watu wengi walikuwa wakitoa sadaka katika sanduku lenye tundu ndogo linalomlazimisha mtoaji kuisukuma noti kwenye tundu hilo na hatimae kushika ubao wa juu wa sanduku hilo kitendo ambacho kinafanywa na waumini wengi katika kutoa sadaka na hatimae waumini hao kutonawa mikono na kisha kurejea tena kwaajili ya kula ekarsti takatifu.
Mh. Wangabo amesema kuwa pamoja na Kanisa kuacha utaratibu wa kutakiana amani ili kuepuka kushikana mikono lakini kwa kitendo hicho cha kila mmoja kugusa kisanduku cha sadaka inakuwa ni namna nyingine na kutakiana amani bila ya waumini wenyewe kutambua.
“Nasema hivyo kwasababu wakati wa kutoa sadaka, haya masanduku kila mtu aliyashika, alishika aking’ang’ana atumbukize hela yake pale kwenye kile kishimo kidogo hivi, si kushika huko umegusagusa pale,na mwengine akaja akashika hapo hapo, kila mtu hapa ndani ameshika tumetakiana amani kwa namna hiyo, ndio maana yake, hii ni hatari sana, lakini pia baada ya kwishashika kile kisanduku kila mtu tumekuja kupokea hapa (Ekaristi) hatujanawa mahali popote, hakuna ndoo (ya maji) hakuna Sanitizer mahali popote, hatukunawa tumeweka mkono, halafu tukaweka mdomoni, tutakuwa salama kweli?” Alihoji.
Na kushauri kuwa masanduku hayo yawe na mdomo mkubwa kiasi cha mtu kuweka hata kwa kutupia akiwa mbali na kutahadharisha kuwa wanaohusika na kuhesabu fedha hizo ni muhimu wakachukua tahadhari kutokana na kutojua fedha hizo zilikotoka kutokana na mzunguko mkubwa wa fedha hizo ndani ya nchi.
“Tunawe mikono yetu kwa sabuni vizuri sana, tuhesabu halafu tuzipeleke benki, kwahiyo Baba Paroko ujihadhari san ana hizi pesa hizi, ziende benki na matumizi yaende kupitia mitandao ya simu, hali sio nzuri, na misongamano tuache, naona hapa namna Watoto walivyokaa mpaka chini, ni vyema mkafanya utaratibu hata Watoto wakawa na misa yao,” Alishauri.
Aidha, alitahadharisha kuwa isitokee makanisa yetu yakawa chanzo cha Corona na kuonya kuwa endapo itafikia hatua hiyo, serikali itatafakari upya ruhusa yake ya kuruhusu madhehebu mbalimbali ya dini kumwabudu na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwenye misikiti na makanisa na hivyo kuwaasa waepuke misongamano.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Emanuel Mtika amewataka waamini hao kuhakikisha kuwa wanakuwa na vifaa vya maji tiririka ikiwemo ndoo zenye koki ama vibuyu chirizi kwaajili kunawa mikono mara nyingi iwezekanavyo na kuwashauri kufika katika kituo cha kutolea huduma ya afya endapo mtu atakuwa anajihisi dalili za mafua makali na sio kuyasubiri mafua hayo yapone yenyewe kama ilivyo kawaida ya watu wengi.
“Kuna ndugu zetu wagonjwa wapo majumbani, na kuna ule utaratibu wetu ukiugua unasubiri uzidiwe ndio unakwenda kutibiwa, kwa kipindi hiki cha Corona kama kuna mgonjwa yeyote aliyomo nyumbani au popote, mpelekeni kwenye kituo cha kutolea huduma, na wewe kama ukiona dalili za namna hiyo zinatokea kama homa, mafua, unapiga chafya, kikohozi kichoeleweka, nenda kwenye kituo cha afya, zahanati ama popote inapotolewa huduma ya afya,” Alisema.
Aidha, Baba Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Namanyere Cosmas Makasi amemuhakikishia Mkuu wa mkoa wa rukwa kuwa ushauri wake wameuchukua na wataufanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa waamini juu ya janga la ugonjwa wa Corona katika Wilaya ya Nkasi.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa